Uturuki: Mtu apatikana hai baada ya saa 248 chini ya kifusi
16 Februari 2023Wakati shughuli za uokozi baada ya tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria zikiingia katika ngazi ya ukarabati na msaada wa kiutu, shirika la habari la taifa la Uturuki, THR Haber limearifu kuwa katika kile kinachoonekana kama muujiza mkubwa, binti wa miaka 17 ameokolewa akiwa hai katika mkoa wa Kahramanmaras, baada ya saa 248 chini ya kifusi.
Soma zaidi: Manusura bado wanaendelea kupatikana kufuatia tetemeko Uturuki na Syria
Vile vile wanawake watatu na watoto wawili walipatikana Jumatano wakiwa hai katika mji huo huo ambao uko karibu na kitovu cha tetemeko la Februari 6.
Wafanyakazi wa shughuli za uokozi walishangilia kwa furaha baada ya watu hao kupatikana wakiwa hai, wakati matumaini ya kuwapata wengine walionusurika yakififia kabisa.
Hayo yakiarifiwa, idadi jumla ya vifo kutokana na tetemeko hilo baya la mwanzoni mwa wiki iliyopita imepindukia 42,000 nchini Uturuki na Syria, Uturuki pekee ikipoteza watu zaidi ya 36,100.
Msaada kwa manusra pamoja na ukarabati
Juhudi sasa zinaelekezwa katika kuwapatia mahitaji ya msingi mamilioni ya watu walioathiriwa na tetemeko hilo, wengi wao wakiachwa bila makaazi katika msimu huu wa baridi kali.
Taasisi za afya zinakabiliwa na changamoto kubwa katika kuzuia kutokea kwa magonjwa ya mripuko, wakati miundombinu ya afya na usafi ikiwa imeharibiwa.
Soma zaidi: Uturuki yaahidi ujenzi mpya wa haraka baada ya tetemeko la ardhi
Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema linahofu juu ya majaliwa ya watu wanaoishi katika mikoa ya kaskazini magharibi mwa Syria inayodhibitiwa na waasi, ambayo haiwezi kufikishiwa msaada kirahisi.
WHO imemhimiza rais wa Syria Bashar al-Assad kufungua vituo zaidi kwenye mpaka baina ya Syria na Uturuki, ili misaada zaidi iweze kuingia.
Un yataka karibu milioni 400 kwa ajili ya watu wa Syria
Hapo jana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kupatikana msaada wa kibinaadamu wa dola milioni 397 kwa ajili ya watu takriban milioni 5 katika eneo hilo.
Wakati huo huo, Banki ya Ulaya ya maendeleo na ukarabati imechapisha ripoti inayokadiria kuwa Uturuki itapoteza asilimia 1 ya pato jumla la ndani kutokana na athari za tetemeko hili alfajiri ya Jumatatu iliyopita.
Soma zaidi: Umoja wa Mataifa watoa wito wa kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi,Syria
Imesema hasara hiyo itatokana na kuhamishia raslimali katika kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa, kutoka bajeti ya miundombinu ya kijamii na minyororo ya usambazaji wa huduma na bidhaa.
Benki hiyo imesema tetemeko la ardhi limeathiri pakubwa maeneo ya kilimo na viwanda vidogo vidogo, na kwamba bila shaka mtikisiko katika sekta hiyo utawafikia wadau katika maeneo mengine yanayotegemea na sekta hizo.
Vyanzo: rtre, dpae