Vifaru vya Urusi vyaivamia ardhi ya Ukraine
24 Februari 2022Katika ujumbe aliouchapisha ukurasa wake wa mtandao wa twitter, waziri Dmytro Kuleba amesema, ''Putin ameanzisha uvamizi kamili dhidi ya Ukraine. Miji yenye amani ya Ukraine inakabiliwa na mashambulizi.''
Waziri huyo ameongeza kuwa tukio hilo ni vita vya ukandamizaji, na kuapa kuwa Ukraine itajilinda na itashinda, na kuwakumbusha viongozi wa dunia kuwa wana wajibu na uwezo wa kumsimamisha Putin.
Picha za kamera za usalama zimeonyesha misafara ya magari ya kijeshi ya Urusi ikiingia kwenye ardhi ya Ukraine kutoka katika rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi.
Putin atoa onyo kali
Vikosi vya Urusi vimelenga vituo kadhaa ndani ya Ukraine, wakati huo huo Putin akitoa onyo kwa nchi zinazoweza kuingilia kati, akidai zitakabiliwa na athari ambazo hazijawahi kushuhudiwa.
Kabla ya mapambazuko leo Alhamisi, miripuko mikubwa ilisikika katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev na miji ya mashariki mwa nchi hiyo ya Kharkiv na Odesa.
Soma zaidi: Marekani, washirika waiwekea vikwazo zaidi Urusi
Katika mji wa Kiev kunashuhudiwa msongamano mkubwa wa magari ya raia wanaoukimbia mji huo, na jeshi la Urusi limedai kuwa limeviharibu vituo vyote vya Ukraine vya ulinzi wa anga na viwanja vyote vya jeshi la angani la nchi hiyo katika saa chache baada ya kuanza kwa uvamizi huu.
Zelenskiy awataka wananchi wa Ukraine kubakia watulivu
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ametangaza sheria ya mazingira ya vita, akisema Urusi inailenga miundombinu ya Ukraine, na kuwataka raia wake kubakia majumbani kwa utulivu. Zelenskiy ameongeza kuwa taasisi za ulinzi za Ukraine zinafanya kazi zikishirikiana na washirika wao.
''Muda mfupi uliopita nimezungumza na Rais Biden. Marekani iko tayari kuratibu msaada wa kimataifa. Leo, tunataka utulivu wa kila mmoja wetu, ikiwezekana tukisalia nyumbani, '' amesema Zelenskiy na kuongeza kuwa wanafanya kazi, jeshi linafanya kazi, sekta nzima ya ulinzi na usalama ya Ukraine inafanya kazi.'
Guterres amtaka Putin kusitisha uvamizi
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hiki ndicho kipindi kigumu kabisa tangu alipochukuwa wadhifa wake, na amemuomba rais Vradimir Putin wa Urusi kusitisha uvamizi huu, kwa maslahi ya ubinadamu.
Jeshi la Urusi limesema haliwalengi raia, bali miundombinu ya kijeshi kwa kutumia silaha za kisasa zenye uwezo wa kupatia shabaha bila kosa. Licha ya ahadi hiyo lakini, tayari zipo taarifa za vifo kutokana na uvamizi huu, ikithibitishwa kuwa raia watano wa Ukraine wamekwishauawa.
ape,rtre