1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, washirika waiwekea vikwazo zaidi Urusi

23 Februari 2022

Marekani na washirika wake wametengaza vikwazo zaidi dhidi ya Urusi, kuhusiana na natua yake ya kuyatambua majimbo mawili yaliojitenga Ukraine, na kwamba vikwazo vikali zaidi vinaisubiri ikiwa itafanya uvamizi kamili.

https://p.dw.com/p/47UZG
Brüssel Treffen NATO-Verteidigungsminister
Picha: NATO

Mmoja ya mizozo mibaya zaidi ya kiusalama unajitokeza barani Ulaya baada ya rais Putin kuamuru wanajeshi kuingia katika mikoa ya Donestsk na Luhansk kufanya kile ambacho Putin alikiita kulinda amani.

Marekani imezitaja hatua za Urusi kama mwanzo wa uvamizi, na rais Joe Biden ametangaza vikwazo kuzuwia kile ambacho mataifa ya magharibi yanahofia kuwa ndiyo mwanzo wa uvamizi kamili.

Soma zaidi:Putin asema maslahi ya Urusi hayajadiliwi katikati mwa mzozo wa Ukraine

Hatua hizo zinafuatia nyingine zilizotangazwa Jumanne, zikiwemo Ujerumani kusitisha uidhinishwaji wa bomba la gesi la Urusi, na kuweka vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya mabenki ya Urusi.

BG Ukraine Protest Berlin
Mwanaume akiwa amebeba bango linalosemeka: Simama na Ukraine, akiwa kwenye maandamano karivu na ubalozi wa Urusi mjini Berlin, Ujerumani, Februari 22,2022.Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Lakini hakuna kati ya hatua zilizotangazwa mpaka sasa zinamlenga moja kwa moja rais Vladmir Putin mwenyewe, na wala hazitarajiwi kuwa na athari kali za muda wa kati kwa Moscow, ambayo ina hifadhi ya fedha za kigeni kiasi cha zaidi ya dola za Marekani bilioni 630.

Vikwazo wa Umoja wa Ulaya vinavyoanza kutekelezwa hii leo, vitawajumusha wabunge wote wa baraza la chini la bunge la Urusi waliopiga kura kuyatambua majimbo hayo, kwenye orodha mbaya, kuzuwia mali zao na kuwapiga marufu kusafiri kwenye kanda hiyo.

Soma pia: Maoni: Putin ametangaza vita

Uingiereza pia imetangaza vikwazo vyake vipya dhidi ya Urusi, ambavyo waziri wa mambo ya nje Liz Truss, amevitaja kuwa vikali zaidi. "Vinawalenga watu walio karibu sana na Kremlin, matajiri muhimu. Vinazilenga benki zinazofadhili jehsi la Urusi na benki muhimu zinazoufadhili utawala," alisema waziri Truss.

Vikwazo vikali zaidi?

"Tunahakikisha pia kwamba Urusi haitoweza kuuza dhamana zake kwenye soko la kimataifa, na tuhahakikisha kwmaba vikwazo vitakuwepo pia kwenye mikoa hiyo. Tunawalenga wanasiasa katika bunge la Urusi waliopiga kura kuwezesha utambuzi huo."

Ukraine,  Donezk | Menschen feiern die Anerkennung der Volksrepublik Donezk durch Russland
Magari yaliowekewa bendera za Urusi yakiwa katikati mwa Donetsk wakati wakaazi wakisherehekea baada ya Urusi kutambua uhuru wa jimbo hilo la Ukraine, Februari 22, 2022.Picha: Alexander Ryumin/TASS/dpa/picture alliance

Mataifa ya kigeni yanahofia kwamba Urusi inapanga uvamizi kamili dhidi ya Ukraine, baada ya Putin kutangaza Jumatatu kwamba anatambua uhuru wa majimbo yaliojitenga tangu mwaka 2014 na yanayodhibitiwa na watu ambao mataifa ya magharibi yanawatazama kama mawakala wa Urusi.

Kwa mujibu wa makadirio ya Marekani, Putin amepeleka wanajeshi wapatao laki moja na tisini kwenye mipaka ya Ukraine.

Katika ishara zaidi za kutokea kwa vita kamili, Urusi imetangaza kwamba imeanza kuondoa wanadiplomasia wake kutoka Kyiv, huku Ukraine ikitangaza hali ya dharua itakayodumu kwa siku 30, na kuwasajili jeshini, wanaume wenye umri wa kupigana.

Kwa miezi kadhaa Urusi imeusilisha mzozo huo kama mgogoro hasa kati yake na mataifa ya magharibi, ikitaka uhakikisho wa kiusalama, ikiwemo ahadi ya kutoiruhusu kamwe Ukraine kuwa mwanachama wa jumuiya ya kujihami NATO.

Lakini utambuzi wa uhuru wa majimbo ya Luhansk na Donetsk, ulifuatia na lugha kali zaidi dhidi ya Ukraine, ikiwemo kutoka kwa Putin binafsi, na hivyo kuongeza wasiwasi kwamba hatoishia tu kwenye uingiliaji ndani ya maeneo yaliojitenga.

Chanzo: Mashirika