Vita vyashika kasi Syria, Iran yataka diplomasia kutumika
3 Desemba 2024Mashambulizi hayo yalitokea kwenye vijiji vilivyopo kaskazini mwa jimbo la Deir Al Zor mapema hii leo. Hayo yanafanywa wakati kundi la Hezbollah la Iraq likitoa wito kwa Baghdad kupeleka wanajeshi nchini Syria kuisaidia serikali.
Muungano wa SDF unaoongozwa na waasi wa Kikurdi kaskazini na mashariki mwa Syria, huko nyuma uliwahi kushirikiana na muungano ulioongozwa na Marekani kupambana na kundi linalolojiita Dola la Kiislamu. Muungano huo unadhibiti robo ya nchi ya Syria, ikiwa ni pamoja na visima vya mafuta na maeneo yanayokaliwa na karibu wanajeshi 900 wa Marekani.
Soma pia:Vikosi vya Syria vyaendelea kukabiliana na waasi Aleppo
Hayo yanaarifiwa, huku kundi la Kataeb Hezbollah la nchini Iraq, lenye ushawishi mkubwa na lenye uhusiano na Iran likitoa wito kwa Iraq kupeleka wanajeshi ili kuisaidia serikali ya Syria dhidi ya mashambulizi ya waasi. Kundi hilo limetoa wito huo katika taarifa iliyosambazwa kwenye chaneli za Telegram zenye mafungamano na Iran jana usiku.
Waasi hao hadi sasa wamefanikiwa kuudhibiti mji wa Aleppo, kaskazini mwa Syria, na kuibua wasiwasi wa kisiasa na kiusalama katika taifa jirani la Iraq.
Msemaji wa Kataeb Hezbollah, ambalo ni sehemu ya kile kinachofahamika kama muungano usio rasmi wa kijeshi kati ya Iran, Syria na makundi mengine, amesema kundi hilo bado halijaamua kupeleka wapiganaji wake, na badala yake kuiomba Baghdad kufanya hivyo.
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian jana usiku alisema magaidi wasipewe nafasi ya kuvianzisha tena vita na umwagaji damu, akiwalenga waasi hao wa nchini Syria.
"Hatutakiwi kuruhusu magaidi na kwa mara nyingine kuanzisha vita na umwagaji damu kwenye ukanda wetu. Tunalazimika kufanya hivi kupitia diplomasia na uratibu na mataifa jirani. Sisi ni ndugu na Waislamu na mataifa mengine," alisema Pezeshkian.
Alisema hayo kwenye mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha televisheni cha taifa.
Anatoa matamshi haya wakati taifa lake likikabiliwa na shinikizo kubwa, katikati ya upungufu mkubwa wa nishati, mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira, huku washirika wake wa kikanda Hamas na Hezbollah wakiwa vitani dhidi ya Israel.
Soma pia: IDF lashambulia "miundombinu ya kijeshi" ya Hezbollah, likisema wanakiuka makubaliano
Katika hatua nyingine, idara ya huduma za dharura inayosimamiwa na upinzani nchini Syria ya "Kofia Nyeupe" siku ya Jumatatu ilisema watu watatu waliuawa katika shambulizi lililofanywa na Urusi kwenye hospitali iliyoko Idlib, wakati mapigano yakizidi kushika kasi. Imesema wawili walikufa baada ya vifaa vya kuwasaidia kupumua kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kuzimika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hadan Fidan amesema jana kwamba, hali hii kwa ujumla inaashiria kwamba Rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad anatakiwa kukubaliana na watu wake na kufanya mazungumzo na upinzani. Alisema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari, sambamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, na kuongeza kuwa Uturuki, Iran pamoja na Urusi wamekubaliana kurejesha juhudi za kidiplomasia, ili kurejesha utulivu nchini Syria.