Vikwazo vya kiuchumi vya ECOWAS kuwaathiri raia wa Niger
31 Julai 2023Chama cha Demokrasia na Ujamaa nchini Niger (PNDS) kimesema mawaziri wanne nchini humo, waziri wa zamani na mkuu wa chama cha rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum wamekamatwa na utawala wa kijeshi, huku chama hicho kikitoa wito wa viongozi hao kuachiliwa mara moja, na kusema Niger inakabiliwa na hatari ya kuwa na kile ilichotaja kuwa "utawala wa kidikteta na wa kiimla."
Kamatakamata hiyo inakwenda sambamba na tamko la utawala wa kijeshi lililowataka mawaziri wote wa zamani na wakuu wa taasisi kurejesha mapema leo mchana magari ya serikali waliyokuwa wakitumia.
Soma pia: Utawala wa kijeshi wa Niger waituhumu Ufaransa kutaka kuuangusha
Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS imewapa wiki moja watawala wa kijeshi ili kuachia madaraka na pia imewawekea vikwazo vikali, ikiwa ni pamoja na kusitisha shughuli zote za kibiashara na kifedha kati ya nchi wanachama na Niger.
Vikwazo vya kiuchumi vinaweza kuwa na athari kubwa kwa watu wa Niger, ambao wanaishi katika nchi ya tatu kwa umaskini zaidi duniani, kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa. Jambo alilosisitiza leo Waziri Mkuu wa Niger Ouhoumoudou Mahamadou:
"Vikwazo hivi vilivyowekwa na mataifa ya Afrika Magharibi vitatasabaisha matatizo makubwa ya kijamii. Kwa raia, litakuwa janga kwa sababu Niger ni nchi inayotegemea mno ushirikiano wake na Jumuiya ya Kimataifa, nchi marafiki na taasisi za kimataifa, ambazo hutoa msaada mkubwa."
Ombi la Niger la mkopo wenye thamani ya dola milioni 51 limetupiliwa mbali hii leo na Benki ya ukanda huo kutokana na vikwazo hivyo vya ECOWAS.
Msimamo wa Ufaransa
Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imesema leo kuwa mamlaka pekee ambayo Ufaransa inaitambua kuwa halali nchini Niger ni ya Rais Mohamed Bazoum. Wizara hiyo haikuthibitisha au kukana ilipoulizwa iwapo Ufaransa ilipewa idhini na Niger ya kufanya mashambulizi ili kumkomboa rais Bazoum aliyepinduliwa madarakani.
Wanajeshi wa Niger walionyakua mamlaka wiki iliyopita wameituhumu hii leo serikali iliyopinduliwa kuwa ilidhinisha kitendo cha Ufaransa kuweza kufanya mashambulizi hayo kwa nia ya kumkomboa na kumrejesha madarakani rais Bazoum.
Hata hivyo Ufaransa imesema inatoa kipaumbele kwa usalama wa raia na ofisi zao, ambazo hazitakiwi kulengwa na vurugu kulingana na sheria za kimataifa. Hapo jana, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisisitiza kuwa nchi yake itachukua hatua iwapo raia au maslahi yake yatahujumuiwa nchini Niger.
Soma pia: ECOWAS kuwawekea vikwazo watawala wa kijeshi Niger
Ujerumani kwa upande wake imesema hii leo kuwa inawasiliana na watawala nchini Niger kutathmini hali halisi ya wanajeshi wake walioko nchini humo. Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema wanajeshi waliohusika na mapinduzi huko Niger wameahidi kuzingatia makubaliano yote ya kimataifa.
Kupinduliwa kwa marais waliochaguliwa kidemokrasia katika mataifa ya Sahel kama Mali, Burkina Faso na Niger kumekuwa kukiambatana na maandamano makubwa ya kuipinga Ufaransa na kuiunga mkono Urusi. Hisia za watu ni kwamba Ufaransa imeshindwa kuwalinda dhidi ya uasi wa makundi ya kigaidi, wakiamini kuwa Urusi itakuwa mshirika wa kuaminika zaidi.