Viongozi wa dini Uganda wataka uchaguzi uahirishwe
23 Desemba 2020Viongozi wa kidini wamejitokeza na wazo hili wakisema kuna changamoto nyingi ambazo zinashughulikiwa kwa sasa hasa kudhibiti ugonjwa wa COVID-19. Wanapendekeza katiba ifanyiwe mageuzi madogo ili Rais Yoweri Museveni aendelee kutawala katika kipindi cha miaka mitatu.
Visa vya makabiliano kati ya polisi, majeshi na wagombea urais katika kipindi hiki cha kampeni vimeishia katika vifo na majehara. Isitoshe matamshi ya vitisho na matusi ambayo yanasikika kutoka kwa baadhi ya wagombea yanasababisha hofu miongoni mwa wananchi kama uchaguzi mkuu utafanyika kwa amani na uhuru.
Polisi wajitetea dhidi ya madai ya kutumia nguvu nyingi
Polisi imesisitiza azma yao ni kuhakikisha kuwa watu wanafuata mwongozo wa kudhibiti ugonjwa wa COVID-19, ila wagombea ndio wanawasababisha kutumia nguvu za kupindukia ikiwemo kufyatua risasi na kurusha mabomu ya kutoa machozi.Ni kutokana na hali hiyo ndipo viongozi wa dini ya Kikristo chini ya jukwaa lao UJCC, wana mtazamo kuwa kwa sababu wagombea wameshindwa kutii mwongozo uliowekwa dhidi ya maambukizi wakiendesha kampeni zao, afadhali zoezi hilo lisifanyike kwa sasa ili kulinda afya ya wananchi.
Pendekezo laibua maoni mseto
Pendekezo hilo la kuahirisha uchaguzi kwa miaka mitatu limepokelewa kwa maoni mbalimbali. Baadhi wanaoliunga mkono wakisema ndiyo njia pekee ya kuhifadhi amani na utangamano pamoja na kudhibiti kasi ya ongezeko la idadi ya watu wanaoambukizwa ugonjwa wa COVID-19.
Lakini wengine wana mashaka kuwa hii ni njia mojawapo ya kumpa Museveni fursa ya kujiimarisha zaidi ili aweze kushinda uchaguzi kwa sababu kwa sasa mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine anampa upinzani mkali na wakati mgumu.
Kulingana na katiba ya Uganda, pakitokea haja ya kuahirisha uchaguzi mkuu, spika wa bunge ndiye huchukua wadhifa wa kiongozi wa serikali.
Hata hivyo hili laweza kuwa jambo gumu kutekeleza katika mazingira ya sasa ya utawala wa Uganda ambapo rais ana mamlaka na ushawishi mkubwa hata katika jeshi ambapo hatua hiyo inaweza kutafsiriwa kama njia ya kumuondoa madarakani.
Pendekezo la katiba kufanyiwa marekebisho
Ni kwa ajili hii ndipo viongozi wa kidini wanapendekeza katiba ifanyiwe mageuzi madogo ili Rais Museveni aendelee kutawala katika kipindi hicho cha miaka mitatu.
Lakini kwa maoni yao, baadhi ya wananchi wanasema hilo ni suala nyeti ambalo kwa sasa litaleta mabishano makubwa na kuitimbukiza nchi katika hali ya taharuki. Aidha, wawekezaji wa kigeni na biashara nyingi watasitisha mipango yao na hivyo kuuathiri uchumi wa nchi.
Ikumbukwe kuwa mataifa kama Tanzania na Burundi yameweza kuendesha uchaguzi katika kipindi hiki cha COVID-19. Hata katika nchi ya Kenya shughuli za kisiasa zinazosababisha mikusanyiko zinaendelea kushuhudiwa. Hadi sasa takriban watu 220 wameripotiwa kufariki kutokana na COVID-19, huku 27,500 wakipimwa na kugunduliwa kuwa na virusi vya corona. Lubega Emmanuel DW Kampala.