Viongozi wa muungano tawala Ujerumani kufanya majadiliano
6 Novemba 2024Migogoro kuhusu jinsi ya kufufua uchumi unaoyumba na kutengeneza bajeti finyu imepamba moto kati ya Chama cha Scholz cha Social Democratic (SPD) na washirika wake wadogo, chama cha Kijani na Free Democratic (FDP).
Baada ya msururu wa mazungumzo ya dharura, viongozi hao wanakutana leo jioni katika ofisi ya Kansela mjini Berlin. Waziri wa Fedha Christian Lindner wa chama kinachoegemea sera za kibiashara - FDP anataka mageuzi mapana ya kiuchumi na hata akatamka wazo la kujiondoa serikalini kabla ya uchaguzi unaopangwa Septemba mwaka ujao.
Soma pia:Vyama vya serikali ya muungano Ujerumani vyakutana kujaribu kutatua mgogoro
Ikiwa ataondoka, hii inaweza kuzusha uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa mapema, pengine mwezi Machi -- au kuwaacha Scholz na chama cha Kijani wakijaribu kusalia madarakani katika serikali ya walio wachache hadi msimu wa kiangazi mwaka ujao.
Mzozo huo umeongeza hali ya sintofahamu katika taifa hilo kubwa zaidi kiuchumi barani Ulaya katika wakati ulimwengu ukisubiri matokeo ya uchaguzi wa Marekani kwa hofu na vita vikiendelea nchini Ukraine na Mashariki ya Kati.