Viongozi wa Umoja wa Ulaya kukutana Albania
6 Desemba 2022Umoja wa Ulaya unataka kuutumia mkutano huo wa kilele wa siku moja unaofanyika kwenye mji mkuu wa Albania, Tirana, kuwaambia viongozi kutoka Albania, Bosnia, Kosovo, Montenegro, Macedonia Kaskazini na Serbia kwamba wana mustakabali ndani ya jumuiya hiyo tajiri ya kiuchumi pamoja na kuwapa ishara madhubuti, badala ya ahadi tu.
Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, mwezi Februari, Mkuu wa Sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borell amekuwa akirejea kusema kuwa kuzidisha ushirikiano wa umoja huo na mataifa hayo sita ni muhimu zaidi kuliko hapo awali, ili kudumisha usalama wa Ulaya.
Mvutano waongezeka eneo la Balkan
Huku uhusiano kati ya Ulaya na Urusi ukizorota kwa sababu ya vita, mvutano pia umeongezeka katika mataifa ya Balkan na Umoja wa Ulaya unataka kuepusha uadui mwingine karibu na mipaka yake.
Kulingana na rasimu ya tamko litakalopitishwa katika mkutano huo wa kilele, Umoja wa Ulaya utarudia ahadi yake kamili na isiyo na mashaka kwa mtazamo wa uwanachama wa Umoja wa Ulaya wa mataifa ya Balkan Magharibi na pia kutoa wito wa kuharakishwa kwa mazungumzo ya kijuinga na viongozi walio madarakani. Na kwa upande wake, Umoja wa Ulaya unatarajia kupata mshikamano kamili kutoka kwa washirika wake wa eneo la magharibi mwa Balkan na kuwataka walingane linapokuja suala la sera zake za kigeni.
Suala hilo limekuwa tatizo kwa Serbia, ambayo Rais wake, Aleksandar Vucic anadai anataka kuiingiza Serbia katika Umoja wa Ulaya, lakini ameimarisha uhusiano wake na Urusi. Ingawa mchakato wa mataifa hayo sita kuelekea kupata uwanachama wa Umoja wa Ulaya ulikuwa umekwama katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na maendeleo kadhaa katika miezi michache iliyopita.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Albania, Edi Rama ameukosoa Umoja wa Ulaya kwa kujikokota katika kujitanua, huku hatua za nchi za magharibi mwa Balkan kujiunga na umoja huo zikikwama kwa miaka mingi. ''Sikuwahi kuifikiria Ulaya kama mashine ya kutoa fedha benki, ATM. Siku zote nimeifikiria Ulaya kama sehemu yenye uhuru na usalama kwa wote,'' alifafanua Rama.
Uhamiaji na mawasiliano pia kujadiliwa
Miongoni mwa hatua madhubuti zitakazopitishwa mjini Tirana, ni kutangazwa kwa mkataba unaohusisha wahusika wa kampuni za mawasiliano ambao watapunguza gharama za kutumia data za mitandao mingine. Mazungumzo hayo pia yataangazia masuala ya uhamiaji, ushirikiano pamoja na athari za nishati na usalama zilizosababishwa na vita vya Urusi nchini Ukraine.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen tayari ametangaza msaada wa kifedha ili kuzisaidia nchi za Balkan Magharibi kukabiliana na uhaba pamoja na bei ya juu ya mafuta. Mara ya mwisho Umoja wa Ulaya kumpokea mwachama mpya Croatia ambayo ni sehemu ya Balkan, ilikuwa mwaka 2013 na kabla ya hapo Bulgaria na Romania zilijiunga na umoja huo mwaka 2007. Kujiondoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya mwaka 2021, umoja huo sasa una mataifa 27 wanachama.
(AP, DPA, Reuters)