Vita vya Gaza vyasababisha mtengano kati ya serikali na umma
5 Januari 2009Viongozi wa Kiarabu wanaitazama hali hiyo kwa wasiwasi mkubwa,kwani maandamano hayo sasa hayafanywi kuzipinga Israel na Marekani tu bali ni dhidi ya serikali zao pia.
Si wote wanaounga mkono mashambulizi ya makombora ya Hamas wala siasa za kundi hilo lenye itikadi kali za Kiislamu.Lakini mashambulizi katili katika Ukanda wa Gaza yaliopindukia kiasi yanaufungamanisha umma wa Kiarabu-Waislamu na jamii zingine wanaandamana pamoja.Jambo jingine linalowafungamanisha ni hasira yao dhidi ya serikali zinazoendelea na kazi zao kama kawaida tu kama anavyoeleza Amr Hamzawy wa Taasisi ya Carnegie mjini Beirut.Yeye anasema,serikali nyingi hutazama upande mwingine-hizo ni serikali zinazosemekana kuwa ni za wastani-yaani Misri,Jordan,Saudi Arabia na nchi zingine za Ghuba.Anaongezea:
"Serikali hizo zingependa kuona nguvu za kisiasa za Hamas zikipunguzwa katika Ukanda wa Gaza sawa na nguvu zake za kijeshi ambazo hata kabla ya uvamizi wa Israel zilikuwa dhaifu."
Kwa maoni ya Hamzawy,viongozi wa nchi hizo za Kiarabu hawaonyeshi utashi- ukimya wao ndio husababisha hasira miongoni mwa waarabu na raia wengine.Serikali za Kiarabu zinazounga mkono mataifa ya magharibi na kujulikana kama serikali za wastani huyatazama makundi kama Hamas au Hezbollah kama ni changamoto kubwa na kitisho kwa hali iliyopo sasa hivi.Mara nyingi serikali hizo huitegemea Marekani kwa misaada ya uchumi na kijeshi.Kati ya serikali hizo hakuna hata moja iliyochaguliwa kidemokrasia.
Hivi karibuni mwandishi mmoja wa habari wa Kuwait alisema "Maangamizi ya Gaza yanaonyesha sura mbaya ya baadhi ya serikali za Kiarabu zilizopoteza heshima ya mwisho iliyokuwepo." Wakati huo huo,Abdul Beri Atwan wa gazeti la Kiarabu "Al Quds al Arabi" anasema,hakuna anaetaka vita kuanzishwa dhidi ya Israel,lakini Waarabu wangeteka,wangeweza kufanikiwa kuleta mabadiliko katika sera za Marekani na Ulaya kuhusu Mashariki ya Kati kwani nchi hizo zina karata nzuri.
Kwa mfano jumuiya ya kimataifa inapigana vita viwili isivyoweza kushinda huko Iraq na Afghanistan.Marekani na Ulaya zinahitaji msaada wa Waarabu kujitoa vitani.Halafu kuna mzozo wa uchumi na fedha na hapo ni nchi za Kiarabu pekee zilizokuwa na fedha za kuyasaidia madola ya Magharibi.Vile vile kuna ushirikiano wa usalama kupiga vita ugaidi.Kwa maoni ya Atwan Waarabu wangeweza kuonya kuwa hawatoshirikiana nao wakati ambapo watu wao wanauawa.
Hakuna hakika ikiwa Hamas itavunjwa nguvu zake kama serikali hizo zinavyotumaini kwa siri. Linalojulikana ni kwamba serikali hizo za Kiarabu zinazoitwa za wastani hazizungumzi kwa niaba ya umma wake.