Vita vya Ukraine vimeupindua mfumo wa dunia - Olaf Scholz
19 Januari 2023Katika hotuba yake Kansela Scholz amesema uvamizi wa Urusi ambao ulifanyika siku chache tu baada ya kumalizika kwa kongamano kama la kimataifa kuhusu uchumi la mwaka jana, ulikuja wakati dunia ilipokuwa ikitarajia ukuaji wa uchumi wa kiwango kizuri, huku mipango ya kuhamia katika nishati safi kwa mazingira ikiwa imeshika kasi.
Soma zaidi: Guterres:Tuwajibike ili kuwa na dunia salama
Amesema baada ya uvamizi huo, nchi nyingi, Ujerumani ikiwemo zilijikuta zikipambana na changamoto ya kuacha utegemezi wa nishati kutoka Urusi, mchakato ambao ulisababisha mfumko wa bei na kupanda kwa gharama ya maisha.
Fursa ya kupata vyanzo mbadala vya nishati
Hata hivyo, amesema kiongozi huyo wa serikali ya Ujerumani, machungu haya yanaweza kuambatana na fursa adimu ya kuipa kisogo nishati chafu kwa mazingira, na yameifanya Ujerumani iache kuitegemea Urusi kama chanzo kikuu cha nishati yake.
''Katika muda wa miezi michache, Ujerumani iliweza kuachana kikamilifu na utegemezi kwa gesi, mafuta na makaa ya mawe kutoka Urusi,'' amesema Scholz, na kuongeza kuwa Ujerumani ilikamilisha ushirikiano na nchi za Asia, Afrika na America ili kupunguza utegemezi huo, ''na naweza kusema kuwa tuko salama lihusikapo suala na nishati mnamo majira haya ya baridi.''
Zelenskiy aongeza shinikizo kutaka Ukraine ipatiwe vifaru
Hotuba nyingine muhimu katika kongamano hili la Davos ilitolewa kwa njia ya vidio na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, ambaye alijikita zaidi katika ombi la nchi yake kutaka ipatiwe vifaru vya kisasa kutoka washirika wake wa magharibi, akionekana kuilenga Ujerumani ambayo licha ya shinikizo kutoka kwa washirika wake katika jumuiya ya kujihami ya NATO, bado inasitasita kuridhia kupelekwa kwa vifaru chapa Leopard-2 nchini Ukraine. Vifaru hivyo hutengenezwa nchini Ujerumani.
Madawa ya kulevya, tatizo sugu
Viongozi wengine waliozungumza jana jioni ni pamoja na rais wa Colombia Gustavo Petro ambaye alikosoa vikali mkakati wa Marekani katika kupambana na madawa ya kulevya. Akichangia juu ya suala hilo kwenye jukwaa lililowashirikisha wanasiasa kutoka Amerika Kusini, rais huyo alisema mkakati huo wa Marekani umesababisha kufungwa jela kwa maelfu ya watu, wengi wakiwa Wamarekani weusi, na wapatao milioni kuuawa katika ukanda wa Amerika Kusini.
Soma zaidi:Davos mjadala watawala ushirika wa China kimataifa
Amesema ikiwa dunia haitakuwa tayari kuwa na mjadala kuhusu sera hiyo ya Marekani iliyoshindwa, dawa za kulevya zitaendelea kuwa tatizo sugu. Yeye alipendekeza mkakati wenye msingi katika kuelimisha, kuzuia na kuwapa matibabu wale ambao tayari wameanguka katika uraibu wa dawa hizo.
Vyanzo: ape, dpae