1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, ukandamizaji waongezeka Ukingo wa Magharibi?

13 Septemba 2024

Wakati macho ya ulimwengu yakielekezwa katika vita vinavyoendelea huko Gaza, eneo la Ukingo wa magharibi lililo umbali wa maili 80 tu linashuhudia vitendo vya ukandamizaji

https://p.dw.com/p/4kc44
Gari la jeshi la Israel likiwa limezuwa gari la wagonjwa kwa ajili ya ukaguzi.
Gari la jeshi la Israel likiwa limezuwa gari la wagonjwa kwa ajili ya ukaguziPicha: RONALDO SCHEMIDT/AFP

 Operesheni ya miezi kadhaa ya jeshi la Israel dhidi ya wale wanaodaiwa kuwa waasi, imesababisha vifo vya makumi ya vijana wa Kipalestina wanaouawa kwa kupigwa risasi na kukamatwa kiholela. 

Zaidi ya vijana 150 walio na umri wa miaka 17 au chini ya hapo, wameuawa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel, eneo lililokumbwa na misukosuko tangu mashambulizi ya Oktoba 7 mwaka jana ambapo Hamas ilivamia kusini mwa Israel na kuwa chanzo cha vita vya Gaza. 

Tangu wakati huo watu wengi wamekuwa wakiuawa eneo hilo kufuatia uvamizi wa karibu kila siku wa jeshi la Israel. Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limeikosoa Israel kwa kutumia nguvu zisizo na uwiano na zisizo halali.

Soma pia:Israel yaua makumi baada ya kushambulia maeneo ya Palestina

Amjad Hamadneh alimpoteza mtoto wake wa kiume kwa jina la Mahmoud wakati shule ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 15 ilipowataka wanafunzi kurejea majumbani mwao kufuatia uvamizi wa mwanzoni mwa mwezi Mei.

Baba huyo ambaye ni fundi ujenzi, anasema mwanaye aliyekuwa mpenzi wa michezo ya kwenye kompyuta hakufanya kosa lolote lakini alikuwa miongoni mwa vijana wawili waliuawa asubuhi hiyo na askari wa Israel.

Kutokana na taarifa kutoka kwa jeshi la Israel,  kwa waasi na hata familia katika Ukingo wa Magharibi, ni wazi kwamba idadi kadhaa ya vijana wa Kipalestina waliouawa katika miezi ya hivi karibuni walikuwa wanachama wa makundi ya wapiganaji.

Wengine wengi waliuawa wakati wa maandamano au kutokana na wao ama mtu aliyekuwa karibu nao kurusha mawe au vilipuzi kwenye magari ya jeshi la Israel.

Lakini imedhihirika kuwa wapo wengine waliouawa kwa kulengwa  na bila sababu yoyote ya msingi, ambapo mauaji kama hayo yanaibua maswali muhimu kuhusu kushuka kwa thamani ya maisha ya vijana wenye kiu ya uhuru na usalama.

Israel: Tumeongeza kasi ya oparesheni

Jeshi la Israel limesema katika taarifa iliyotumwa kwa shirika la habari la Associated Press kwamba imeongeza idadi na kasi ya operesheni zake tangu Oktoba 7 ili kuwakamata wanamgambo wanaoshukiwa kufanya mashambulizi katika Ukingo wa Magharibi na kusisitiza kwamba "wote" waliouawa katika kipindi hiki ama walikuwa na silaha au walishiriki katika vitendo vya kigaidi wakati wa tukio.

Shambulizi la roketi lauwa watu 12 katika milima ya Golan

Kambi ya wakimbizi ya Jenin ambayo kwa muda mrefu imekuwa na sifa mbaya ya kutambulika kama kitovu cha wanamgambo wa Kipalestina, imekuwa ikivamiwa mara kwa mara na wanajeshi wa Israel tangu walichukua udhibiti wa Ukingo wa Magharibi wakati wa vita vya mwaka 1967 kati ya Israel na nchi jirani za Kiarabu.

Eneo hilo linalokaliwa kimabavu na Israel lilishuhudia mapigano mabaya hata kabla ya vita hivyo kuanza. Lakini wanajeshi na polisi wa Israel wanaojaribu kuwadhibiti Wapalestina milioni 3 na wenye jukumu la kuwalinda walowezi wa Kiyahudi wapatao 500,000, wameongeza kiasi ya vitendo vyao vya uvamizi katika miezi ya hivi karibuni.

Soma pia:Shambulizi la Israel lawaua watu 40 katika eneo salama linalokaliwa na Wapalestina

Vijana wanawakilisha karibu robo ya Wapalestina takriban 700 waliouawa katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita vya Gaza, ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu maandamano makubwa ya kupinga ukatili na uvamizi wa kigeni yanayofahamika kama Intifadha ya Pili mwanzoni mwa miaka ya 2000. 

Lakini pia zaidi ya raia 20 na wanajeshi kadhaa wa Israel wameuawa katika eneo hilo tangu mwezi Oktoba mwaka 2023. Msemaji wa jeshi la Israel alisema kuwa jeshi hilo haliwalengi raia na hufanya juhudi kubwa kuepuka kuwadhuru wakati wa operesheni zao na kwamba mashirika ya kutetea haki za binadamu huzingatia na kuangazia matukio machache.