Von der Leyen aizuru Ukraine kujadili usalama wa nishati
20 Septemba 2024Majadiliano hayo ni muhimu ikizingatiwa kwamba sehemu kubwa ya miundombinu ya nishati ya Ukraine imeharibiwa na mashambulizi ya Urusi tangu kuanza kwa vita miaka miwili na nusu iliyopita.
Ziara ya Von de Leyen mjini Kyiv inafanyika baada ya kushuhudiwa makabiliano makali wakati wa msimu wa kiangazi unaoelekea ukingoni ambayo yamesababisha uharibifu wa kutisha kwenye mifumo ya nishati ya Ukraine.
Kati ya mwezi Mei hadi sasa vikosi vya Urusi vimekuwa vikisonga mbele upande wa Mashariki mwa Ukraine huku wanajeshi wa Kyiv wakiendelea kuishikilia sehemu ya ardhi ya Urusi waliyoikamata wakati wa shambulizi lao la kushtukiza mnamo mwezi Agosti.
Katika ujumbe wake kupitia mtandao wa X aloutuma muda mfupi baada ya kuwasili Kyiv kwa treni akitokea Poland, Bibi Von der Leyen amesema anafanya ziara yake ya 8 nchini Ukraine katikati ya hujuma nzito za Urusi dhidi ya miundombinu ya uzalishaji na usambazaji nishati ya Ukraine. Amesema Umoja wa Ulaya umedhamiria kuisaidia Ukraine kuvuka msimu wa baridi salama.
Amearifu kwamba analenga kutumia mazungumzo yake na Rais Volodoymyr Zelenskyy kujadili maandaalizi kuelekea msimu huo pamoja na msaada wa kifedha ambao nchi hiyo unaweza kuupata kutoka Kundi la mataifa tajiri la G7.
IEA yatahadharisha kuwa msimu wa baridi utakuwa mgumu zaidi kwa Ukraine
Hapo jana Shirika la Kimataifa la Masuala ya Nishati IEA lilitoa hadhari kwamba msimu wa baridi wa mwaka huu utakuwa "mgumu zaidi" kwa Ukraine, kwa sababu miundombinu ya nishati ya nchi hiyo imesambaratishwa na kampeni ya kijeshi ya Urusi.
Mkuu wa IEA Fatih Birol aliwasilisha mpango utakaoisaidia Ukraine kuilinda gridi yake ya taifa akisema ni "lazima kuwasaidia watu wa Ukraine kupata joto".
Misimu miwili ya baridi iliyopita tangu vita vilipozuka vita ilishuhudia maelfu ya watu nchini Ukraine wakiishi bila umeme au vipasha joto majumbani kutokana na kuhujumiwa vituo vyake vya kufua na kusambaza nishati hiyo muhimu.
Ziara ya Von der Leyen mjini Kyiv inajiri katikati ya miito ya nchi hiyo ya kuyataka mataifa ya magharibi yairuhusu kutumia makombora ya masafa kuyapiga maeneo ya ndani mwa Urusi.
Maombi hayo yalizusha hamaki mjini Moscow, na Ikulu ya Kremlin imekwishaonya itaizingatia hatua hiyo kuwa ni kujihusisha moja kwa moja kwa mataifa ya magharibi na Jumuiya ya NATO kwenye mzozo huo.
Urusi yazitaka nchi za magharibi kuacha kuipatia silaha Ukraine
Mapema hii leo wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imeyataka mataifa ya magharibi kusitisha mara moja kuipatia Ukraine silaha na kufadhili kile imekitaja kuwa "shughuli za kigaidi". Msemaji wa wizara hiyo Maria Zakharova amesema ikiwa nchi za magharibi zimedhamiria kupata suluhisho la vita vya Ukraine upelekaji silaha ni lazima ufike mwisho.
"Kila mtu: (iwe ni) waandishi wa kimataifa, wataalamu wa siasa na hata mtu wa kawaida anaweza kupata jibu litakalothibitisha dhamira ya kisiasa na kidiplomasia. Pale nchi za magharibi zitakapoacha kuupatia silaha utawala mjini Kyiv na kufadhili shughuli za kigaidi, hilo litakuwa ishara kwamba wanataka suluhu ya kidiplomasia" amesema Zakharova.
Matamshi hayo ya Zakharova yumkini ni ujumbe kutoka Moscow kwamba iwapo Ukraine haitoacha kupigana, hakutakuwa na amani. Yametolewa wakati Rais Zelenskyy wa Ukraine anajiandaa hivi karibuni kwa ziara nchini Marekani atakayoitumia kuwasilisha mapendekezo yake ya jinsi ya kumaliza vita nchini mwake.
Duru zinasema akiwa mjini Washington, Zelenskyy atakutana na Rais Joe Biden na wagombea wawili wa kiti cha urais wa Marekani, Kamala Harris na Donald Trump.