1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waaustria wazikataa siasa kali za mrengo wa kulia

6 Desemba 2016

Nchi za Umoja wa Ulaya zilivuta pumzi ya furaha pale Norbert Hofer, alipokubali kuwa ameshindwa na mgombea wa kujitegemea aliyekuwa anaungwa mkono na Chama cha Kijani, Alexander Van der Bellen.

https://p.dw.com/p/2Tk9T
Österreich Präsidentschaftswahlen Alexander Van der Bellen
Picha: Reuters/L. Foeger

Wananchi wa Austira wamekatisha ndoto ya urais ya Norbert Hofer ambaye kama angelishinda angekuwa rais wa kwanza katika nchi za Umoja wa Ulaya anayelemea siasa kali za mrengo wa kulia, siasa ambazo zina mtazamo mkali kuhusu wahamiaji na vilevile kuuangalia Umoja wa Ulaya kuwa ni chombo ambacho sio cha uhakika sana.  

Badala yake mgombea wa kujitegemea, Alexander Van der Bellen, aliweza kuzoa asilimia 53.3 ya kura dhidi ya mpinzani wake Norbert Hofer wa kutoka chama cha Freedom FPO aliyepata asilimia 46.7.  

Van der Bellen alisema kuwa anaona rangi za bendera ya Austria "Nyekundu, nyeupe na nyekundu kuwa ni alama ya matumaini kutoka Vienna hadi katika miji mikuu yote ya nchi za Umoja wa Ulaya."

Ulaya yawapongeza Waaustria

Baada ya ushindi huo wa Van der Bellen, viongozi mbali mbali wa umoja wa Ulaya wameelezea furaha yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amesema kuwa ana furaha sana kutokana na matokeo ya uchaguzi wa Austria ambao amesema ni ishara nzuri dhidi ya siasa kali za mrengo wa kulia zinazoshika kasi katika bara ya Ulaya.

Kwa upande wake, Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema ameukaribisha ushindi wa mgombea ambaye anaelemea siasa za mrengo wa shoto pia alimpongeza Van der Bellen kwa kushinda kwa asilimia kubwa dhidi ya mpinzani wake ushindi ambao hauna shaka, Hollande amesema ushindi huo unadhihirisha mshikamano na kuvumiliana kwa bara la Ulaya.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk, amesema katika taarifa yake kuwa wakati ambapo bara la Ulaya linakabiliwa na changamoto nyingi, mchango wa Austria katika kutafuta suluhisho la pamoja la Ulaya na umoja uliopo ni jambo la muhimu.  

Wakati yote hayo yanapoendelea mgombea mtarajiwa wa urais nchini Ufaransa, Marine le Pen, amempongeza Norbert Hofer na kumpa moyo kuwa uchaguzi utakaokuja atashinda.

Le Pen na Hofer wote wanalemea siasa kali za mrengio wa kulia na wanaupinga Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf