Wafungwa 6,000 watoroka gereza lenye ulinzi mkali Msumbiji
27 Desemba 2024Mkuu wa polisi Msumbiji amesema wafungwa takriban 6,000, wakiwemo 29 waliokuwa wamehukumiwa kwa ugaidi, walitoroka kutoka Gereza Kuu la Maputo siku ya Krismasi wakati wa maandamano yenye vurugu, kufuatia uthibitisho wa ushindi wa chama tawala cha Frelimo katika uchaguzi mkuu uliopita.
Mkuu huyo wa polisi Bernadino Rafael, amesema wafungwa 33 walikuda na wengine 15 walijeruhiwa wakati wa makabiliano na vikosi vya usalama. Maandamano hayo, yaliyofanywa na wafuasi wa mgombea aliyeshindwa Venancio Mondlane, yalisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya polisi na kuanguka kwa ukuta wa gereza.
Soma pia: Watu 21 wauawa katika machafuko Msumbiji baada ya uamuzi wa mahakama
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji Pascoal Ronda ameyahusisha machafuko hayo na mzozo wa matokeo ya uchaguzi, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa wito wa mazungumzo na kukomesha vurugu. Wafungwa wengi waliotoroka tayari wamekamatwa tena.