1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waingereza kuamua kama wabakie au wajiondoe EU

23 Juni 2016

Mamilioni ya Waingereza leo wanapiga kura ya maoni ya kihistoria kuamua kama wabakie au wajiondoe katika Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1JBlg
Picha: Reuters/A. Yates

Wapiga kura wengi wamejitokeza kusini-mashariki mwa Uingereza kupiga kura, bila ya kujali mvua kubwa na radi ambayo imesababisha foleni ndefu ya watu wanaosubiri kupiga kura katika mitaa ya London.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa tangu saa moja kamili asubuhi kwa saa za Uingereza katika maeneo ya England, Wales, Scotland na Ireland Kaskazini na vinatarajiwa kufungwa majira ya saa nne usiku.

Watu milioni 46.5 wajiandikisha

Kiasi ya watu milioni 46.5 idadi ambayo imevunja rekodi, wamejiandikisha kupiga kura hiyo yenye ushindani mkali kabisa kuamua kama Uingereza isalie au ijiondoe kwenye Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28, ambao ulianzishwa kwa dhamira ya kuungana na kuwa na amani ya kudumu, baada ya maafa ya vita viwili vikuu vya dunia.

Pindi watakapofika kwenye vituo vya kupigia kura, wataulizwa swali moja tu kwenye karatasi za kupigia kura: iwapo Uingereza ibakie mwanachama wa Umoja wa Ulaya au ijiondoe kwenye umoja huo.

David Cameron na mkewe, Samantha
David Cameron na mkewe, SamanthaPicha: Reuters/S. Wermuth

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron tayari ameshapiga kura yake katika kituo kilichoko karibu na makazi yake, Downing Street, katikati ya London. Cameron anayetaka Uingereza ibakie kwenye Umoja wa Ulaya, aliongozana na mkewe, Samantha. Cameron amewasihi Waingereza kupiga kura ya kubakia kwenye umoja huo.

Kwa upande wake kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour, Jeremy Corbyn amesema ana matumaini kwamba kambi yake inayounga mkono Uingereza kubakia kwenye Umoja wa Ulaya itashinda. Akizungumza wakati akiwasili kupiga kura, Corbyn amesema leo ni siku nzuri kwake na anajiamini.

Mchuano ni mkali

Utafiti wa mwisho wa maoni uliotolewa jana usiku unaonyesha kuwa asilimia 45 ya Waingereza wanataka kujiondoa katika Umoja wa Ulaya na asilimia 44 wanataka kubakia. Asilimia 9 ya Waingereza bado hawajaamua. Utafiti huo uliwahusisha zaidi ya watu wazima 3,000.

Waziri Kiongozi wa Scotland, Nicola Sturgeon
Waziri Kiongozi wa Scotland, Nicola SturgeonPicha: Reuters/C. Kilcoyne

Matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutangazwa mapema kesho asubuhi, huku ikielezwa kuwa matokeo rasmi yatatangazwa mida ya saa moja kamili jioni.

Waziri Kiongozi wa Scotland, Nicola Sturgeon amesema kama Uingereza itajiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, basi naye anapendekeza Scotland iitishe kura ya maoni ya kujitenga na Uingereza.

Nayo mabenki ya kimataifa yameonya kuwa thamani ya Pauni inaweza ikashuka kwa kasi, kama Uingereza itapiga kura ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya na wafanyabiashara watarajie kuwa katika hali tete zaidi kuliko muda wowote ule tangu ulipozuka mzozo wa kifedha mwaka 2008 na 2009.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,DPA,RTR
Mhariri: Yusuf Saumu