1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu wajihisi hawako salama UIaya

4 Desemba 2023

Vita kati ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza vimesababisha waumini wa dini ya Kiislamu barani Ulaya kuishi na wasiwasi mkubwa, huku huku takwimu zikionesha ongezeko la chuki na uhasama dhidi yao.

https://p.dw.com/p/4ZlTX
Maandamano ya kupinga mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Maandamano ya kupinga mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Michael Kuenne/PRESSCOV/ZUMA/picture alliance

Vitendo vya chuki, ambavyo pia ni uhalifu, vimeongezeka mno barani Ulaya tangu shambulio la Oktoba 7 ambapo kundi la Hamas liliwauwa takribani Waisraeli 1,200, huku Wapalestina zaidi ya 14,800 wakiuawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel katika Ukanda wa Gaza. 

Sio tu chuki dhidi ya Waislamu, lakini pia matukio yaliyorekodiwa ya chuki dhidi ya Wayahudi yameongezeka kwa asilimia 1,240 mjini London nchini Uingereza.

Hali hiyo imeshuhudiwa pia katika mataifa mengine ya Ulaya kama vile Ufaransa na Ujerumani.

Soma zaidi: Israel yalegeza mashambulizi yake Gaza kwa saa 3 kwa siku.

Ingawa takwimu rasmi zinaonesha ongezeko dogo la matukio ya chuki dhidi ya Waislamu katika mataifa hayo, lakini data hizo hazikuzingatia kikamilifu mashambulizi dhidi ya watu binafsi na misikiti, wakiwemo watoto wanaolengwa mashuleni.

Jian Omar, mbunge wa jimbo la Berlin mwenye asili ya Kikurdi kutoka Syria, anahisi kutopewa ulinzi wa kutosha na polisi baada ya kioo cha ofisi yake kuvunjwa na kupokea pia vipeperushi vilivyojaa chuki vilivyochanganywa na vigae na kinyesi huku mshambuliaji akimtishia na nyundo.

Maandamano ya kudai usitishwaji mapigano kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika Berlin, Ujerumani, siku ya Jumamosi (Disemba  2).
Maandamano ya kudai usitishwaji mapigano kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika Berlin, Ujerumani, siku ya Jumamosi (Disemba 2).Picha: Michael Kuenne/PRESSCOV/ZUMA/picture alliance

Madhila yaliyomkuta Omar ni miongoni mwa matukio yanayoongezeka ya chuki dhidi ya Waislamu barani Ulaya ambayo, kwa kiasi fulani, yanachochewa na wanasiasa tangu mashambulizi ya Hamas.

Imani ndogo kwa polisi

Zaidi ya viongozi 30 wa jamii na mawakili waliozungumza na shirika la habari la Reuters walisema matukio mengine mengi hayaripotiwi kwa sababu ya watu kuwa na imani ndogo kwa polisi.

Omar alisema anajihisi mpweke huku akihoji kuwa "ikiwa mbunge hawezi kulindwa, hali itakuwa vipi kwa raia wa kawaida?"

Mbunge huyo alisema polisi walimueleza kuwa wanaendelea na uchunguzi, lakini wakamwambia hawawezi kutoa ulinzi wa ziada kwenye ofisi yake.

Soma zaidi: Majeshi ya Israel yavamia Gaza

Omar aliibua mjadala na kuhoji ingekuwaje kama ingelikuwa mwanasiasa mzungu wa Ujerumani aliyeshambuliwa na "mhamiaji au mkimbizi?"

Polisi wa Berlin hawakutaka kuelezea chochote juu ya taarifa hii.

Maandamano ya kudai usitishwaji mapigano kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika tarehe 2 Disemba 2023 mjini Düsseldorf.
Maandamano ya kudai usitishwaji mapigano kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika tarehe 2 Disemba 2023 mjini Düsseldorf.Picha: Thomas Banneyer/dpa/picture alliance

Zara Mohammed, katibu mkuu wa Baraza la Waislamu wa Uingereza, anasema kauli ya serikali ya kuyaita maandamano ya kuiunga mkono Palestina "maandamano ya chuki," imesababisha hisia mseto kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi au haki za Waislamu. 

Zara alisema mawaziri hawakuwa makini hasa kwa kusababisha mivutano ya kitamaduni na kutenganisha jamii na kusema kuwa hilo halisaidii bali huleta mgawanyiko ulio hatari.

Serikali ya Uingereza haikujibu chochote kuhusu matumizi rasmi ya lugha kama hiyo.

Wasiwasi waongezeka

Hali ya Waislamu wa Ulaya kujihisi kutokuwa salama imeongezeka pia baada ya chama cha mrengo mkali wa kulia nchini Uholanzi (PVV) kushinda uchaguzi wa bunge wiki iliyopita, ambapo mwenyekiti wake, Geert Wilders, amekuwa akidhihirisha wazi chuki dhidi ya Waislamu na kutoa wito wa misikiti na Qur'an kupigwa marufuku nchini humo.

Maandamano ya kudai usitishwaji mapigano kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika tarehe 2 Disemba 2023 mjini Düsseldorf.
Maandamano ya kudai usitishwaji mapigano kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika tarehe 2 Disemba 2023 mjini Düsseldorf.Picha: Thomas Banneyer/dpa/picture alliance

Hata nchini Marekani, kumekuwa kukiripotiwa ghasia na mashambulizi dhidi ya Wapalestina tangu Oktoba 7.

Soma zaidi: Vita vya Israel-Hamas: IDF yatanua mashambulizi ya ardhini Gaza

Katika Msikiti wa Ibn Ben Badis katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, kwa sasa wazee wanaogopa kuhudhuria Sala ya Alfajiri baada ya kupokea vitisho mwishoni mwa mwezi Oktoba kuwa msikiti huo ungelichomwa moto, na inaonekana vitisho hivyo vilitolewa na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.

Kundi la kampeni la "Mwambie Mama" limeripoti kuwa majaribio ya kuchoma moto, matusi, uharibifu na vichwa vya nguruwe kutupwa kwenye eneo la msikiti ni miongoni mwa matukio zaidi ya 700 ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza, mwezi mmoja baada ya kuanza kwa mzozo wa Mashariki ya Kati, ikiwa ni ongezeko la hadi mara saba ukilinganisha na mwezi uliopita.