1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani wengi ni masikini - Utafiti

13 Desemba 2024

Utafiti unaonesha kuwa licha ya kuishi kwenye taifa kubwa kabisa kiuchumi la Umoja wa Ulaya na nchi ya kundi la mataifa saba yaliyoendelea kwa viwanda duniani (G7), watu wengi nchini Ujerumani ni masikini.

https://p.dw.com/p/4o7ht
Watu wakipatiwa misaada ya vyakula nchini Ujerumani.
Watu wakipatiwa misaada ya vyakula nchini Ujerumani.Picha: Thomas Lohnes/Getty Images

Kutokana na kupanda viwango vya kodi za nyumba na gharama nyengine za makaazi, familia nyingi nchini Ujerumani hutumia zaidi ya robo ya pato lao kwenye kulipia makaazi, huku wengine wakitumia zaidi ya nusu.

Utafiti uliofanywa na jumuiya ya misaada ya kiutu iitwayo Paritätische Gesamtverband kwa maagizo ya Ofisi Kuu ya Takwimu ya Ujerumani na matokeo yake kuchapishwa siku ya Ijumaa (Disemba 13) unaonesha kuwa baada ya kutowa gharama za kodi ya nyumba, riba za madeni na gharama nyengine za lazima, zaidi ya watu milioni 17.5 husalia na kiasi kidogo cha fedha ama hawabakii na chochote, hali inayowaweka kwenye mstari wa umasikini.  

Umasikini unavyowatesa wastaafu Germany

Ujerumani inamtambua mtu kuwa kwenye umasikini ikiwa kwenye mapato yao ya mwezi wanasaliwa na chini ya asilimia 60 ya pato la chini. Pato la chini ni lile ambalo nusu ya watu hupata zaidi na nusu yake hupata chini yake. 

Kwa mujibu wa utafiti huo, mamilioni ya watu hawaonekani kwenye takwimu kwa sababu gharama za nyumba hazijumuishwi kwenye hisabu ya mapato na matumizi.

"Ikiwa mtu anaangalia tu kwenye mapato, lakini sio ukweli kwamba watu wanasalia na fedha chache sana kwa sababu ya gharama kubwa ya makaazi, atakuwa anakipuuzia kiwango cha umasikini nchini Ujerumani." Ilisema ripoti ya utafiti huo.

Masikini zaidi ya ilivyokisiwa

Utafiti huo unaonesha kuwa watu milioni 5.4 zaidi wanaishi chini ya kiwango cha umasikini nchini Ujerumani kuliko ilivyokisiwa awali. Ikiwa gharama za makaazi zinajumuishwa kwenye hisabu ya mapato na matumizi, basi zaidi ya asilimia 20 ya watu nchini Ujerumani wanachukuliwa kuwa masikini.

Utafiti: Kiwango cha Umasikini Ujerumani bado kipo juu

Uchambuzi wa ripoti hiyo unaonesha kuwa vijana walio chini ya umri wa miaka 25, wakiwemo wanafunzi, na watu wazima walio na umri wa kuanzia miaka 65 na zaidi wameathirika zaidi na kile kiitwacho umasikini wa makaazi.

Wale wanaoishi peke yao wanaathirika zaidi kuliko wanaoshi pamoja, kwani hubeba gharama zote peke yao. Na hali inatajwa kuzidi kuwa mbaya kwa wastaafu wanaoishi peke yao.

Hata hivyo, kuna tafauti baina ya majimbo: majimbo ya Bremen, Saxony-Anhalt na Hamburg yana umasikini mkubwa zaidi wa makaazi, huku hali ikiwa afadhali kwenye majimbo ya Baden-Württemberg na Bavaria. 

Kutokana na hayo, mkurugenzi mkuu wa shirika la Paritätische Gesamtverband, Joachim Rock, ameitaka serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi wa mwezi ujao, kuandaa sera maalum ambayo itazuwia umasikini kwa kutowa mishahara mizuri, mfumo bora zaidi wa ustawi wa jamii na kodi za nyumba ambazo zinastahmilika.