1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaguzi wa kimataifa wa nyuklia waelekea Zaporizhzhia

31 Agosti 2022

Timu ya wakaguzi wa Shirika la Kimataifa la kudhibiti matumizi ya Nishati ya Nyuklia, IAEA inatarajiwa kuwasili katika kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia Alhamisi asubuhi.

https://p.dw.com/p/4GGFh
Ukraine | IAEA in Kiew
Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Shirika la habari la Urusi, TASS limeripoti Jumatano kuwa timu hiyo inayoongozwa na mkurugenzi mkuu wa shirika la IAEA, Rafael Grossi, baada ya kuwasili itafanya ukaguzi kwa muda wa siku moja au mbili. Likiwanukuu maafisa waliowekwa na Urusi katika mji wa Enerhodar ambako kinu hicho kipo, TASS imesema kuwa wataalamu wapatao sita hadi wanane wa IAEA wanatarajiwa kubakia katika kinu hicho baada ya ziara hiyo.

Ujumbe huo wa IAEA uliwasili mjini Kiev jana jioni. Grossi amesema ana matumaini ya kuweka wataalamu wa kudumu nchini Ukraine kwa ajili ya kukifuatilia kinu hicho kikubwa kabisa cha nishati ya nyuklia barani Ulaya.

Zelensky: Urusi inashambulia kabla ya wakaguzi kuwasili

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema Urusi inayashambulia maeneo yaliyo karibu na kinu hicho kinachodhibitiwa na Urusi, tangu mwezi Machi, kabla ya kuwasili kwa ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa. Zelensky amesema ana matumaini kwamba ujumbe huo utafanikiwa kuanza kutekeleza shughuli zake.

''Huu ni ujumbe muhimu na tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha unakuwa katika eneo salama. Kwa bahati mbaya, Urusi inaendelea na vitendo vyake vya uchokozi katika maeneo ya karibu na kinu hicho, ambacho lazima ujumbe huo ufike hapo. Lakini nina matumaini kwamba ujumbe wa IAEA utaweza kufanya shughuli zake,'' alisisitiza Zelensky.

Huku hayo yakijiri majeshi ya Ukraine yameendelea kuvishambulia vikosi vya Urusi katika mashambulizi yaliyoanza Jumatatu ya kulikomboa eneo lake la kusini. Uingereza, ambaye ni mshirika wa karibu wa Ukraine imesema kuwa vikosi vya Ukraine vilivyoko eneo la kusini vimeyarudisha nyuma majeshi ya Urusi yaliyokuwa mstari wa mbele katika maeneo kadhaa ya mapambano.

Ukraine-Krieg | Kämpfe in der Region Cherson
Eneo la maduka makubwa katika jimbo la Kherson likiwa limeshambuliwaPicha: STRINGER/AFP/Getty Images

Mshauri wa Rais wa Ukraine, Oleksiy Arestovych amesema vikosi vya Ukraine vinashambulia kwa makombora meli zinazotumiwa na Urusi kusafirisha vikosi vyake kwenye ukingo wa Mto Dnipro. Urusi kwa upande wake imesema vikosi vya Ukraine, baada ya kujaribu kuingia katika maeneo matatu tofauti ya mapambano kwenye majimbo ya Mykolaiv na Kherson, vimepoteza wanajeshi 1,200 pamoja na vifaru 139, magari ya kivita na malori.

Kuleba ataka Warusi wazuiwe kuingia Ulaya

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba amesema Umoja wa Ulaya unapaswa kuwapiga marufuku watalii wa Urusi kuingia katika nchi za umoja huo. Amewataka mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Prague kuchukua hatua hiyo. Hata hivyo, nchi za umoja huo zimegawanyika kuhusu uamuzi wa kuwanyima visa wananchi wa Urusi wanaotaka kuingia Ulaya. 

Ama kwa upande mwingine, Urusi imesema Jumatano kuwa serikali ya Ujerumani inafanya kila iwezalo kuharibu uhusiano wake wa nishati na Urusi, saa chache baada ya kampuni ya nishati ya Urusi, Gazprom kulifunga bomba kubwa linalosafirisha gesi kutoka Urusi kwenda Ulaya kwa ajili ya kufanya matengenezo.

Matengenezo hayo kwenye bomba la gesi la Nord Stream 1 linaloziunganisha Urusi na Ujerumani kupitia Bahari ya Baltic, yatafanyika kwa siku tatu kuanzia Alhamisi, hivyo hakutakuwepo na gesi inayoingina Ujerumani kati ya Agosti 31 hadi Septemba 3.

(AFP, DPA, Reuters)