1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Ukraine wapindukia milioni 11

5 Aprili 2022

Umoja wa Mataifa unakisia kwamba zaidi ya watu milioni 11 wameshayakimbia makaazi yao nchini Ukraine tangu uvamizi wa Urusi uanze, huku mashambulizi yakizidi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/49Ur8
Ukraine | Zerstörungen in Mariupol
Picha: Privat

Kwenye tathmini yake ya kwanza ndani ya kipindi cha wiki tatu, Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) lenye makao yake makuu mjini Geneva, Uswisi, lilisema siku ya Jumanne (5 Aprili) kwamba zaidi ya watu milioni saba wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani ya Ukraine yenyewe kufikia tarehe 1 Aprili. 

Idadi hii ni kando ya wengine zaidi ya milioni nne ambao wamekimbilia nje ya nchi, huku wengine wanaokaribia milioni tatu wakiwa mbioni kuchukuwa uamuzi wa kukimbia vita kwenye makaazi yao, kwa mujibu wa IOM.

Idadi hii ni ongezeko la takribani watu milioni mbili ikilanganishwa na ya katikati mwa mwezi Machi, ambapo watu wapatapo milioni tisa na nusu walikuwa wameshakimbilia nje ama kwenye maeneo mengine ndani ya Ukraine. 

Kabla ya uvamizi wa Urusi kuanza mnamo mwezi Februari, Ukraine ilikuwa na wakaazi milioni 44. 

Mashambulizi yashamiri ndani ya Ukraine

Ukraine-Krieg | Eindrücke aus Butscha
Mashambulizi yanaendelea kuyabomoa majengo na maeneo mbalimbali Ukraine.Picha: State Emergency Service in Kyiv Oblast/REUTERS

Taarifa hiyo inatolewa huku ndani ya Ukraine yenyewe hali ikizidi kuwa mbaya. Siku ya Jumanne, gavana wa jimbo la mashariki la Luhansk aliwataka wakaazi kujifungia majumbani mwao na kuvaa barakowa zenye unyevunyevu baada ya kombora la Urusi kupiga kifaru kilichobeba tindikali.

Akitumia mtandao wa Telegram, Serhiy Haidai aalisema mashambulizi hayo yalitokea karibu na mji wa Rubizhne, ambao jeshi la Ukraine linasema Warusi wanataka kuudhibiti. 

Watoto nchini Ukraine wahofia kifo

Gavana huyo amesema tindikali hiyo ya sumu ni hatari endapo watu watavuta hewa yake, ama inapogusana na ngozi na majimaji ya mwili.

Urusi haijazungumzia tukio hilo, ambalo shirika la habari la Reuters linasema halijaweza kuthibitishwa na vyanzo huru.

Mkuu wa majeshi wa Ukraine amesema asubuhi ya leo kwamba Urusi inavipanga upya vikosi vyake kwa ajili ya uvamizi katika eneo la Donbas, kwa lengo la kuwa na udhibiti wa moja kwa moja wa majimbo ya Luhansk na Donetsk yaliyotangaza kujitenga na Ukraine. 

Meli ya raia yashambuliwa Mariupol

Bilderchronik des Krieges in der Ukraine l Zerstörtes Haus südlich von Mariupol
Jengo lililobomolewa kwa mabomu ya Urusi mjini Mariupol.Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Katika tukio jengine, mamlaka nchini Ukraine ziliripoti kuzama kwa meli ya abiria katika bandari ya mji uliozingirwa wa Mariupol, baada ya vikosi vya Urusi kuirushia makombora.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ukraine ilisema meli hiyo inayopeperusha bendera ya Jamhuri ya Dominica ilipigwa kombora kutokea baharini, lakini walifanikiwa kuwaokowa mabaharia wake.

Jeshi la Urusi limeuzingira na limekuwa likiushambulia mji huomuhimu wa bandari kwa wiki tatu mfululizo. Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema linatazamia leo kufanikiwa kwenye mji huo kuratibu misaada ya kiutu, baada ya wafanyakazi wake kuzuiwa usiku wa jana wakiwa umbali wa kilomita 20 magharibi wa mji huo.

Shirika hilo ambalo limekuwa likijaribu kuwa na kikosi chake ndani ya Mariupol tangu Ijumaa iliyopita, lilisema kikosi hicho kilishikiliwa na polisi kwenye mji wa Manhush, lakini kiliachiwa usiku wa kuamkia leo.