Wakristo duniani kote washerehekea sikukuu ya Krismasi
25 Desemba 2024Usiku wa kuamkia leo, mamia ya watu walikusanyika katika kanisa la Uzawa kwenye mji wa Bethlehem ambao ni mji mtakatifu kwa Wakristo.
Hata hivyo ni mwaka wa pili mfululizo ambapo sherehe za Krismasi zinaadhimishwa kwenye mji wa Bethlehem bila mapambo, huku idadi ya wageni ikizidi kuwa ndogo ikilinganishwa na hapo zamani. Hali ya huzuni imetanda kwenye mji wa Bethlehem kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Katika Uwanja wa Manger, katikati ya mji huo wa Wapalestina unaojulikana kwa kanisa takatifu linaloaminika kuwa eneo alikozaliwa Yesu Kristo, kundi la maskauti lilifanya maandamano madogo leo asubuhi na kwa mwaka wa pili sasa, mti mkubwa wa Krismasi katika Uwanja wa Manger haukuwashwa mataa kusisitiza huzuni iliyopo.