1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Wanafunzi 200 walazwa hospitali Uganda

21 Julai 2023

Zaidi ya wanafunzi 200 wa shule moja ya sekondari nchini Uganda wamelazwa hospitali baada ya kula chakula kisicho salama usiku wa kuamkia jana Alhamisi.

https://p.dw.com/p/4UDdD
DW Eco Africa-Sendung (23.09.2022)
Picha: DW

Taarifa za awali za polisi zinaelezea kuwa sampuli zimepelekwa kwenye maabara ya serikali kuchunguza chakula walichokula wanafunzi hao na kuwasababishia hali ya maumivu na kuharisha. 

soma pia: Mkuu wa WFP aelezea wasiwasi kuhusu usalama wa chakula Afrika

Kulingana na wasimamizi wa shule hiyo ya kibinafsi, wanafunzi zaidi ya 200 walianza kuelezea kukumbwa na maumivu baada ya kula ugali na maharage jumatano jioni. Usiku kucha walianza kuharisha na ilibidi magari ya wagonjwa kuitwa na wakakimbizwa katika hospital kuu ya Nagalama. Kulingana na afisa mkuu wa matibabu wilaya ya Mukono Dkt Stephen Mulindwa, huenda wanafunzi hao walikula chakula ambacho hakikuwa salama katika mazingira kilivyowekwa au kutayarishwa.

Soma pia: Moto uliowaua wanafunzi 19 uliwashwa na mwanafunzi

Wazazi wa watoto hao walikimbilia shule hiyo ya bweni kutaka kujua hali za watoto wao baada ya habari kusambaa kwamba walikuwa wamefariki. Ila mkuu wa shule hiyo Amos Balongo amekanusha madai hayo akisema kuwa wanafunzi wanaendelea vyema baada ya kutibiwa na wataruhusiwa kurudi nyumbani.

Chakula kinavyoandaliwa

Ätiopien | Markt in Bahir Dar
Picha: Alemenew Mekonnen/DW

Kulingana na wataalamu, chakula kutokuwa salama inatokana na jinsi kinavyoshughulikiwa katika mnyororo kuanzia shambani hadi kinapopakuliwa mezani. Hata kutumia vyombo vichafu kama sahani kunaweza kusababisha madhara kwa walaji. Ni kwa ajili hii ndipo wanatahadharisha kila mhusika katika mchakato wa kuandaa chakula kuhakikisha kuwa chakula hakichuliwi na kemikali na vitu vingine visivyo salama. 

Soma pia: Wanafunzi watatu kati ya 6 waliotekwa nyara na kwenye shule ya bweni magharibi mwa Uganda wafaulu kutoroka na kujiwasilisha kwa jeshi la Uganda.

Huku wakisubiri matokeo kutoka kwa maabara ya serikli, wasimamizi wa shule hiyo wamelezea kuwa hawmshuku mtu yeyote kwa sasa kwa kuhusika katika hila ya kusababisha chakula cha wanafunzi hao kutokuwa salama. Hadi wakati wa kuandaa ripoti hii baadhi ya wanafunzi walikuwa wameruhusiwa kuondoka hospitali.