1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Monusco kuondoka Kongo ifikapo Disemba

Jean Noël Ba-Mweze
24 Oktoba 2023

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imejulisha kwamba tume ya Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, itaanza kujiondoa mwishoni mwa mwezi Disemba.

https://p.dw.com/p/4XwqW
Baada ya miaka 25 nchini Kongo, kikosi cha Monusco kimetarajiwa kuondoka ifikapo Disemba
Baada ya miaka 25 nchini Kongo, kikosi cha Monusco kimetarajiwa kuondoka ifikapo DisembaPicha: Olivia Acland/REUTERS

Waziri wa mambo ya nje Christophe Lutundula, aliyasema hayo jana Jumatatu, wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na Patrick Muyaya, Waziri wa Mawasiliano ambae pia ni Msemaji wa Serikali.

Lutundula alieleza kuwa kazi za kuandaa  mpango huo wa Monusco kuondoka zimeanzishwa baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kulikubali ombi la mamlaka ya Kinshasa la kutaka ujumbe huo wa monusco  uondoke hapa nchini.

"Ni mwishoni mwa mwezi wa Disemba ndipo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaamua kuhusu mustakabali wa MONUSCO tangu kuwepo tume hiyo hapa nchini mwetu kufuatana na ripoti iliyotolewa na Katibu Mkuu.'', alisema Lutundula,

Na kuongeza : ''Pia nawajulisha kuwa leo tumeanza na MONUSCO, mchakato wa kuandaa mpango wa kujiondoa ujumbe huo kama sisi Kongo tulivyoomba."

Kazi za kuandaa mpango huo wa Monusco kujiondoa nchini Kongo zinajumuisha wataalam wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na wale wa Umoja wa Mataifa.

Kuna mpango wa kujitenga kwa vikosi vya Monusco

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo, Christophe Lutundula
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo, Christophe LutundulaPicha: Nicolas Maeterlinck/AFP/Getty Images

Wataalam hao wanaandaa nyaraka mbalimbali zikiwemo hizi anazozitaja waziri wa mambo ya nje, Christophe Lutundula. 

"Kuna mpango wa kujitenga kwa vikosi vya MONUSCO, ratiba ya kujiondoa pamoja na mipango ya kivitendo yaani makabidhiano ya kazi, mpango wa kupunguza polepole idadi ya wafanyakazi wa MONUSCO. Pia tutaandaa mpangilio wa ratiba itakayoonyesha jinsi vyombo vya MONUSCO vitaanza kwenda.", alisisitiza Lutundula.

Kwa miaka kadhaa sasa  mamlaka ya Kongo imekuwa  ikiliomba baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuondowa ujumbe wake wa kulinda amani nchini Kongo, huku mamia ya makundi yenye kumiliki silaha yakiendelea kuyumbisha hali ya usalama katika eneo la mashariki mwa hiyo ambapo imeshuhudiwa kila mara wakazi wakiandamana kupinga uwepo wa Monusco.