Wanajeshi wa Marekani washambuliwa Syria
10 Agosti 2024Afisa mmoja wa Marekani ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba kwa sasa wanafanya tathmini ya kitabibu na madhara ya mashambulizi hayo yaliyofanyika kwenye eneo la Rumalyn, waliko wanajeshi wa Marekani na washirika wao.
Haya ni mashambulizi ya pili kwa siku za hivi karibuni, wakati kukiwa na wasiwasi wa mashambulizi makubwa ya Iran na washirika wake, kufuatia mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismael Haniyeh.
Soma: Shambulio la Israel laua wapiganaji wawili wa Hezbollah kusini mwa Lebanon
Iran inaituhumu Marekani kuisaidia Israel kwenye mauaji hayo yaliyofanyika mjini Tehran.
Siku ya Jumatatu, wanajeshi watano wa Marekani walijeruhiwa kwenye kituo cha jeshi la anga cha Ain al-Asad magharibi mwa Iraq, mashambulizi ambayo Pentagon inadai yalifanywa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran.
Marekani ina wanajeshi 900 nchini Syria na 2,500 nchini Iraq, inaodai wanatowa mafunzo kwa vikosi vya nchi hizo kuzuwia kuzuka upya kwa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu.