WASHINGTON-Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia yakutana kumchagua Rais mpya wa Benki hiyo.
31 Machi 2005Bodi ya Wakurugenzi Watendaji ya Benki ya Dunia yenye wajumbe 24,inakutana leo kumchagua mtu atakayekamata nafasi ya Urais wa benki hiyo,inayoachwa wazi na Bwana James Wolfensohn,huku Naibu Waziri wa Ulinzi wa Marekani,Paul Wolfowitz akiwa mgombea pekee wa nafasi hiyo.Kwa kawaida wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Watendaji ya benki ya Dunia hukutana mara moja tu kwa mwaka.
Mataifa ya Umoja wa Ulaya yanaweka shinikizo kubwa kwa Bwana Wolfowitz,kumteua mtu kutoka moja ya nchi ya Ulaya kuwa Naibu wake.
Kwa utaratibu,Rais wa Benki ya Dunia hushikilia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano na huweza kuongezwa miaka mitano mingine.Rais wa sasa wa Benki hiyo,Wolfensohn anamaliza muda wake tarehe 31 mwezi wa machi mwaka huu.
Benki ya dunia mwaka jana pekee ilitoa dola bilioni 20.1,kwa miradi 245 ya maendeleo katika nchi zinazoendelea duniani kote.Pia Benki hiyo ndio mhimili mkubwa wa kusaidia elimu na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI katika sehemu mbalimbali duniani.