Washirika wa Bouteflika watakiwa kuondoka madarakani
5 Aprili 2019Waandamanaji waliobeba mabango yenye maneno ya kudai mabadiliko zaidi, walimiminika katika mji mkuu, Algiers, kwa maandamano yao ya kila Ijumaa hivi leo ikiwa ni mara yao ya saba.
Maandamano ya leo yalifanyika huku kukiwa na taarifa ya kufutwa kazi kwa mkuu wa idara ya ujasusi, hii ikiwa ni dalili ya mgogoro katika uongozi wa juu kufuatia kujiuzulu kwa Bouteflika.
Waandamanaji walipaza sauti zao wakitaka mfumo mzima wa kisiasa ulioundwa chini ya chama tawala, maafisa wa kijeshi, wafanyabiashara, mashirika na wapiganaji wa vita vya uhuru dhidi ya Ufaransa vya mwaka 1954 hadi mwaka 1962 kuondoka.
Hali ya usalama imeimarishwa katika taifa hilo la Afrika ya Kaskazini lililo tajiri kwa mafuta na gesi, huku kukiwa na vizuizi vya barabarani kuyazuwiya mabasi yaliyowabeba waandamanaji wanaoupinga utawala wanaouona fisadi na kandamizi kuingia kwa wingi mjini. Haya ni maandamano ya kwanza tangu Bouteflika alipoondoka madarakani.
Safari hii waandamanaji pia wanamtaka Waziri Mkuu Noureddine Bedoui, spika wa bunge Abdelkader Bensalah pamoja na rais wa mahakama ya katiba, Tayeb Belaiz, wote waondoke mara moja madarakani.
Wapinzani wa washirika wa Bouteflika wasema ni lazima washirika hao waondoke madarakani
Viongozi hawa ni washirika na watu watiifu kwa Bouteflika na ndio ambao sasa wamepewa jukumu la kuongoza kipindi cha mpito baada ya kiongozi wao wa muda mrefu kuondoka madarakani akiwa na miaka 82.
Bensalah, ambaye ni spika wa bunge kwa miaka 16, ndiye atakayekuwa rais wa mpito hadi pale uchaguzi utakapoandaliwa baada ya siku 90. Belaiz, waziri aliyeongoza kwa miaka 16 pia aliteuliwa na Bouteflika kuongoza baraza la katiba litakalosimamia uchaguzi.
Naye Bedoui kabla ya kuchaguliwa kuwa waziri mkuu alifanya kazi kama waziri wa mambo ndani. Wapinzani wao wanasema watu hawa watatu waliojiharibia majina kwa kukaa muda mrefu chini ya uongozi wa Bouteflika wanapaswa kufuata mkondo wake na kujiuzulu.
Huku hayo yakiarifiwa, wanaharakati wanaendelea na mapambanao yao katika mitandao ya kijamii wakitoa wito wa maandamano ya amani na ya furaha ya kuuondoa utawala waliouita wa kidikteta.
Bouteflika alijiuzulu siku ya Jumanne baada ya maandamano makubwa dhidi yake kufuatia hatua yake ya kuwania urais kwa muhula wa tano, licha ya kutoonekana hadharani kwa muda mrefu baada ya kuugua kiharusi mwaka wa 2013.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP/Reuters
Mahriri: Mohammed Khelef