Wasifu wa Moise Katumbi
20 Desemba 2023Maisha binafsi
Moïse Katumbi alizaliwa tarehe 28 Desemba 1964 sasa ana miaka 58. Mama yake ni Mkongo kutoka makabila ya Bemba na Yeke na baba yake, Nissim Soriano ana asili ya Ugiriki. Mzee huyo alikimbia Rhodes 1938 baada ya kuanzishwa utawala wa Kiitaliano wa kifashisti uliokuwa na sheria za ubaguzi wa rangi.
Mzee huyo aliishi katika mji wa Katanga, nchini Kongo wakati huo ilikuwa koloni la Ubelgiji. Katumbi alikulia katika kijiji cha Kashobwe nchini Kongo karibu na Ziwa Mweru karibu na mpaka wa Zambia.
Moïse Katumbi Chapwe ni mfanyabiashara na mwanasiasa. Ni mmoja wa watu matajiri zaidi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alikuwa Gavana wa jimbo la Katanga, lililoko kusini mwa Kongo, kuanzia 2007 hadi Septemba 2015. Alikuwa mwanachama wa Chama cha People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD) hadi Septemba 2015.
Shughuli za kisiasa
Mnamo Januari 2007, Katumbi alikuwa Gavana wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia kuliwakilisha jimbo la Katanga, alipata kura 94 kati ya jumla ya kura 102. Utawala wake umepata sifa kutokana na kuufufua uchumi katika jimbo hilo kupitia hatua za kuendeleza miundombinu, kuhimiza uwekezaji kutoka nje kwa kuweka punguzo la kodi, kupunguza urasimu katika shughuli za serikali, na kupambana na rushwa.
Pamoja na uchimbaji wa madini, Katumbi alilenga kuyapanua maeneo mengine ya uchumi wa jimbo hilo ikiwa ni pamoja na sekta za huduma, nishati na kilimo.
Mnamo Septemba mwaka 2015, Katumbi alijiuzulu ugavana na pia kwenye chama chake cha kisiasa, People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD).
Tarehe 12 Machi 2018, Katumbi alizindua rasmi kampeni yake ya urais pamoja na muungano wake mpya wa kisiasa, Ensemble Pour le Changement (Pamoja kwa Mabadiliko).
Mnamo Desemba 2021, Moïse Katumbi alizindua rasmi chama chake cha kisiasa cha Ensemble Pour la République, katika mji muhimu wa Kisangani ulio kaskazini mashariki mwa Kongo na kutangaza nia yake ya kugombea katika uchaguzi wa rais wa 2023.
Kandanda
Tangu 1997, Katumbi ni rais wa timu ya soka ya TP Mazembe ya mjini Lubumbashi. Timu hiyo imeshinda kombe la Shirikisho la Kandanda barani Afrika, CAF mara tano na kuwa timu ya kwanza barani Afrika kucheza katika fainali za FIFA kombe la dunia mwaka 2010.
Mtazamo wa umma
Kwa ujumla Moise Katumbi anatazamwa vyema katika Jimbo la Katanga na kitaifa kutokana na maendeleo aliyoleta katika eneo la Katanga na pia kama rais wa TP Mazembe. Anajulikana kwa ukarimu wakena pia kwa kuelekeza fedha zake kwa ajili ya kuisaidia jamii.
Mwaka wa 2012 jarida la The African Report, lilimtangaza Moise katumbi kuwa mmoja kati ya "Waafrika 50 wenye ushawishi mkubwa” na mnamo mwaka 2015 jarida la Jeune Afrique, lilimtaja kuwa "Mwafrika Bora wa Mwaka.”
Chanzo: AFP