Wasudani waadhimisha Eid-ul-Fitr katikati ya mabomu
21 Aprili 2023Awali, kikosi cha Jeshi la Dharura, RSF, ambacho kinapingana na jeshi rasmi la Sudan, kilikuwa kimekubaliana na usitishaji mapigano uliotakiwa kuanza saa 10:00 alfajiri ya Ijumaa (Aprili 21) kupisha sherehe za Sikukuu ya Eid el-Fitr na pia kufungua njia kwa ajili ya watoaji wa huduma za kiutu kuwafikia maelfu ya raia waliokwama katikati ya mapigano.
Hata hivyo, jeshi rasmi halikutowa kauli yoyote kuthibitisha ama kukataa usitishaji huo wa mapigano.
Badala yake, kwenye ujumbe wake wa kwanza kwa njia ya video tangu mapigano yaanze wiki iliyopita, mkuu wa majeshi na kiongozi wa sasa wa Sudan, Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, alisema asubuhi ya Ijumaa kwamba bado anataka kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.
Soma zaidi: Sudan: Guterres atoa wito wa kusitishwa mapigano
"Uharibifu na sauti za bunduki hazijawapa watu wetu nafasi ya kusherehekea Eid kama wanavyostahiki, na hilo linatusikitisha. Lakini kuna matumaini kwamba tupo na umma na tutayapita majaribu haya na kuibuka tukiwa wamoja na madhubuti kama ilivyo kaulimbiu yetu: Jeshi moja, umma mmoja. Tuna hakika tutavuuka kwa hekima na uimara utakaoilinda nchi yetu na kuturuhusu kuwa na kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia." Alisema kiongozi huyo.
Hali mbaya Khartoum
Vyombo vya habari viliripoti mashambulizi mapya kwenye mji mkuu Khartoum asubuhi ya leo, huku wanajeshi wakionekana kwenye mitaa inayokaliwa na raia.
Umoja wa Mataifa unasema maelfu ya wakaazi wa mji huo mkuu wamelazimika kujifungia majumbani mwao kwa siku kadhaa sasa, wakiwa hawana maji wala umeme.
Soma zaidi: RSF: Tuko tayari kusitisha mapigano Sudan
Mwandishi wa habari wa shirika la habari la Ujerumani, dpa, anaripoti kuwepo uhaba mkubwa wa chakula, mafuta na madawa wakati maduka machache yakiwa wazi mjini Khartoum, masoko makubwa yamefungwa licha ya kwamba leo ni siku ya kuadhimisha kumalizika kwa mfungo wa Ramadhani.
Korea Kusini kuhamisha raia wake
Hayo yakijiri, Korea Kusini imejiunga kwenye orodha ya mataifa yanayotuma ndege za kijeshi na wanajeshi kuwaokowa raia wake waliokwama nchini Sudan, ambako watu zaidi ya 300 wameshauawa tangu mapigano ya kuwania madaraka yaanze wiki iliyopita.
Soma zaidi: Mapigano Khartoum yatishia kuvunja mpango wa kusitishwa mapigano Sudan
Wizara ya ulinzi ya Korea Kusini imesema kuwa itatuma ndege yake ya kijeshi chapa C-130J, licha ya kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum waliko raia wake umefungwa.
Kwa sasa, kikosi chake cha kijeshi kimewekwa kwenye hali ya utayari katika taifa jirani la Djibouti, kwa ajili ya kufanya operesheni hiyo ya uokozi wakati wowote kutoka sasa.
Mataifa mengine yaliyochukuwa hatua kama hizo ni pamoja na Japan, Marekani na Uholanzi.
Mapigano yalianza siku ya Ijumaa iliyopita kati ya vikosi vya majenerali wawili wenye nguvu sana - Abdel-Fattah al-Burhan na naibu wake, Mohammed Hamdan Daglo.
Wababe hao wawili wamekuwa wakiliongoza taifa hilo la kaskazini mashariki mwa Afrika lenye wakaazi milioni 46 tangu waliposhirikiana kufanya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya mapinduzi ya umma mwaka 2021.
Vyanzo: AFP, dpa