Watawala wapya wa Syria waanza kuwasaka masalia wa Assad
26 Desemba 2024Mamlaka mpya za Syria Alhamisi zilianzisha msako wa usalama katika mkoa wa pwani wa Tartous, ambako maafisa wa polisi 14 waliuawa siku moja kabla, zikiahidi kuwasaka "masalia" wa utawala wa Bashar al-Assad uliopinduliwa, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Ghasia katika mkoa wa Tartous, unaokaliwa na wanachama wengi wa madhehebu ya Alawi, zimekuwa changamoto kubwa zaidi kwa mamlaka mpya zinazoongozwa na makundi ya Kisunni, yalioongoza mashambulizi yalioundoa utawala wa Assad mnamo Desemba 8.
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali, SANA, vikosi vya usalama vya utawala mpya vilianza operesheni ya "kudhibiti usalama, utulivu, na amani ya kijamii, na kuwasaka masalia ya wanamgambo wa Assad kwenye misitu na vilima" vya maeneo ya vijijini ya Tartous.
Soma pia: Vikosi vya Syria vyapata vifo 14 katika mapigano Tartus
Wanachama wa madhehebu ya Alawi, ambayo ni tawi la Uislamu wa Shia, walikuwa na ushawishi mkubwa wakati wa utawala wa Assad, wakitawala vikosi vya usalama vilivyotumika kukandamiza wapinzani wake katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 13 na miongo ya ukandamizaji wa polisi wake.
Katika dalili za mvutano wa kimadhehebu, waandamanaji walisikika wakitoa maneno ya "Ee Ali!" wakati wa maandamano nje ya makao makuu ya serikali ya mkoa wa Tartous, kama ilivyoonyeshwa na picha za mitandao ya kijamii Jumatano.
Kauli hizo zilikuwa zikimaanisha Ali ibn Abi Talib, binamu wa Mtume Muhammad (SAW), anayetukuzwa sana na Waislamu wa Shia na Alawi.
Kundi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS), ambalo liliongoza kampeni ya waasi iliyomuondoa Assad, limeahidi mara kwa mara kulinda makundi ya kidini ya wachache, yanayohofia kwamba utawala mpya unaweza kuanzisha serikali ya Kiislamu yenye msimamo mkali.
Machafuko Homs
Wizara ya Habari ya Syria ilitangaza marufuku ya kusambaza au kuchapisha maudhui yoyote ya vyombo vya habari yenye lengo la kuzua mgawanyiko wa kimadhehebu miongoni mwa Wasyria.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vilichukua sura ya kimadhehebu wakati Assad alipowatumia wanamgambo wa Kishia kutoka kote Mashariki ya Kati, wakihamasishwa na mshirika wake Iran, kupambana na waasi waliotawaliwa na Waislamu wa Sunni.
Upinzani umeibuka pia katika mji wa Homs, kilomita 150 kaskazini mwa Damascus. Vyombo vya habari vya serikali viliripoti kwamba polisi walitangaza kafyu Jumatano usiku, kufuatia machafuko yanayohusiana na maandamano yaliyoongozwa na wanachama wa jamii za Alawi na Shia.
Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Jumatano kutoka Homs zilionyesha umati wa watu wakitawanyika huku milio ya risasi ikisikika. Reuters ilithibitisha eneo hilo, ingawa haikufahamika nani aliyekuwa akifyatua risasi.
Iran na Lebanoni zazungumzia hali ya Syria
Mshirika wa muda mrefu wa Assad, Iran, imekosoa mwelekeo wa matukio nchini Syria katika siku za hivi karibuni. Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, aliwataka vijana wa Syria kusimama imara dhidi ya wale aliowatuhumu kuchochea hali ya kutoelewana.
Hata hivyo, waziri mpya wa mambo ya nje wa Syria, Asaad Hassan al-Shibani, aliitaka Iran kuheshimu mapenzi ya watu wa Syria na mamlaka ya nchi hiyo.
Aliionya dhidi ya kusababisha machafuko zaidi, akisema Iran itawajibika kwa athari zozote za matamshi yake.
Lebanon, Alhamisi, ilitangaza nia ya kuwa na uhusiano mzuri wa ujirani na Syria, ikiwa ni ujumbe wa kwanza rasmi kwa utawala mpya mjini Damascus.
Kundi lake la Hezbollah la Lebanon lilitoa mchango mkubwa kuupiga utawala wa Assad wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, kabla ya kuanza kuondoa wapiganaji wake kutoka Syria kwa lengo la kuimarisha safu zake katika vita dhidi ya Israel.