1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Syria

Polisi 14 wa Syria wauawa shambulio la kuvisia Tartus

26 Desemba 2024

Waziri mpya wa mambo ya ndani wa Syria amesema askari14 wameuawa na 10 kujeruhiwa katika mapigano na wanajeshi wa utawala wa zamani wa Bashar al-Assad karibu na mji wa Tartus.

https://p.dw.com/p/4oZnS
Wapiganaji wa Syria wakijikusanya katika mtaa mmoja mjini Damascus
Wapiganaji wa Syria wakijikusanya katika mtaa mmoja mjini Damascus, usiku wa Desemba 25, 2024.Picha: Leo Correa/AP/dpa/picture alliance

Watu kumi na saba wameuawa Jumatano katika mkoa wa Tartus, Syria, katika mapigano kati ya vikosi vya usalama na watu wenye silaha, wakati maafisa wa utawala mpya wakijaribu kumkamata afisa aliyehusishwa na uhalifu uliotekelezwa chini ya utawala wa Bashar al-Assad uliopinduliwa.

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu Syria liliripoti kuwa wanachama 14 wa Kikosi cha Usalama wa Jumla na watu watatu wenye silaha waliuawa katika mji wa Khirbet al-Maaza.

Afisa huyo, Mohammed Kanjo Hassan, alikuwa mkuu wa idara ya sheria ya kijeshi na alijulikana kwa kutoa hukumu za kifo na maamuzi ya kiholela katika gereza la Saydnaya, maarufu kwa mateso na mauaji ya kiholela.

Polisi wakitoa ulinzi mjini Qamishli, Syria.
Polisi wakitoa ulinzi mjini Qamishli, Syria.Picha: DELIL SOULEIMAN/AFP/Getty Images

Utawala wa mpito ulisema Alhamisi asubuhi kuwa maafisa 14 wa polisi waliuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika "shambulio la kuvizia" lililofanywa na vikosi vya wafuasi wa utawala uliopinduliwa.

Soma pia:Kiongozi mpya wa Syria asema serikali itadhibiti silaha zote 

Waziri mpya wa Mambo ya Ndani wa Syria, Mohammed Abdel Rahman, aliahidi kuchukua hatua kali dhidi ya mabaki ya utawala wa Assad na kulinda usalama wa nchi.

Maandamano na marufuku ya kutembea usiku kucha katika mkoa wa Homs, pamoja na maandamano madogo karibu na pwani, yaliashiria machafuko makubwa zaidi tangu kuondolewa kwa Assad mnamo Desemba 8.

Kafyu yatangazwa Homs

Huko Homs, wakazi waliripoti maandamano yaliyoongozwa na wanachama wa jamii za Alawi na Shia, makundi ya wachache yaliyoonekana kihistoria kuwa waaminifu kwa Assad.

Wizara ya mambo ya ndani ilitangaza kafyu kuanzia saa 12 jioni Jumatano hadi saa mbili asubuhi Alhamisi ili kupunguza ghasia.

Assad akimbia nchi, waasi waukamata Damascus

Ingawa madai ya waandamanaji bado hayajafahamika, baadhi walihusisha machafuko hayo na shinikizo na ukatili wa hivi karibuni dhidi ya wachache wa Alawi.

Video moja iliyoenea mtandaoni, ikionyesha moto ndani ya eneo takatifu la Alawi huko Aleppo pamoja na watu wenye silaha karibu, ilizidisha mvutano.

Wizara ya mambo ya ndani ilikanusha muda wa video hiyo, ikisema kuwa inatokana na mashambulizi ya waasi mnamo Novemba huko Aleppo na kwamba inalenga kuzua mgawanyiko wa kimadhehebu.

Soma pia: Kiongozi mpya Syria aahidi kuheshimu mamlaka ya Lebanon

Utawala mpya unaoongozwa na kundi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) umekuwa ukiahidi mara kwa mara kulinda makundi ya kidini ya wachache katikati ya hofu ya kuanzishwa kwa serikali ya Kiislamu.

Hata hivyo, maandamano katika maeneo ya pwani kama Tartus yanaonyesha mvutano unaoendelea, huku shambulio la kuvizia la Jumatano likiashiria udhaifu wa mamlaka ya utawala wa mpito.

Kufuatia kuondolewa kwa utawala wa Assad na nchi ikikumbwa na mgawanyiko wa kimadhehebu, hatima ya maelfu ya waliopotea na urithi wa miongo ya ukandamizaji vinaendelea kuchochea hali ya kutoelewana.