Watu 11 watiwa mbaroni New Caledonia
20 Juni 2024Polisi katika kisiwa cha Ufaransa cha New Caledonia wamewakamata watu 11 siku ya Jumatano akiwemo kiongozi mpigania uhuru, Christian Tein, ambao wanashukiwa kwa kuwa na jukumu katika machafuko ya umwagaji damu yaliyokigubika kisiwa hicho ambacho wakazi wazawa wa jamii ya Wakanaki kwa muda mrefu wamepigania kujitenga na kuwa huru kutoka kwa Ufaransa.
Ukamataji huo ni sehemu ya uchunguzi wa polisi unaoendelea ambao ulianzishwa mnamo Mei 17, siku chache baada ya machafuko ya kwanza kuzuka na kugeuka kuwa makabiliano ya kutumia silaha, uporaji na machafuko mengine yaliyozigeuza baadhi ya sehemu za mji mkuu, Noumea na vitongoji vyake kuwa maeneo yasiyofikika.
Soma pia: Macron ahimiza vizuizi viondolewe dhidi ya New Caledonia
Mwendesha mashtaka wa New Caledonia, Yves Dupas amesema katika taarifa kwamba operesheni hiyo ya polisi ilianza mapema asubuhi, huku washukiwa wengine wakitiwa mbaroni baadaye mchana, wakiwemo baadhi waliojisalimisha wenyewe kwenye vituo vya polisi.