Zelensky asema Urusi ina sifa za "Dola ya Kigaidi"
29 Juni 2022Kupitia ujumbe wake wa video anaoutoa kila siku kwa umma wa Ukraine, rais Zelensky amesema ni wazi shambulizi kwenye mji wa Kremenchuk liliamriwa na mamlaka za Urusi na lengo lake lilikuwa ni kuwaua watu wengi iwezekanavyo.
Amesema shambulizi hilo ni mwendelezo wa hujuma zinazofanywa na Urusi dhidi ya raia wa Ukraine na ameapa kwamba Moscow itawajibishwa kwa uhalifu huo alioufananisha na ugaidi.
Ameongeza kusema kuwa Urusi inapaswa kuendelea kuadhibiwa kwa vikwazo vikali vya kiuchumi na baadae mbele ya mahakama maalumu ya makosa ya kivita itakayoundwa baada ya kumalizika kwa vita.
Kiongozi huyo alirejea matamshi hayo alipolihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video jana Jumanne na kuwataka wajumbe wa chombo hicho kuchukua hatua kali dhidi ya Urusi kwa ukatili inaoutenda akisema taifa hilo halipaswi hata kuendelea kuwa mwanachama wa Baraza hilo.
"Urusi haina haki ya kuwa sehemu ya majadiliano au kupiga kura kuhusu vita inavyopigana dhidi ya Ukraine ambavyo havikutokana na uchokozi na badala yake ni ukoloni tu wa upande wa Urusi. Ninawarai kuwapokonya wawakilishi wa taifa hilo la kigaidi nguvu zao ndani ya Umoja wa Mataifa na hilo linawezekana na ni muhimu" amesema rais Zelensky.
Hata hivo madai hayo ya rais Zelensky yamepingwa vikali na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov. Amekanusha kwamba siyo kweli nchi yake imelilenga eneo la manunuzi ya vitu kwenye mji wa Kremenchuk na badala yake amedai Moscow iliyashambulia kwa kombora majengo yanayohifadhi silaha zilizotolewa na mataifa ya magharibi kwa Ukraine.
Watu wengine watatu wauwawa huku vita vikiendelea upande wa mashariki
Katika kisa kingine watu watatu wameuwawa hii leo kwenye mji wa kusini mwa Ukraine wa Mykolaiv. Kulinga na gavana wa kijeshi wa jimbo hilo Vitaly Kim kombora lililofyetuliwa na vikosi vya Urusi ndiyo chanzo cha vifo vya watu hao.
Mamlaka za jimbo hilo zimewatolea wito raia kubakia kwenye mahandaki ya kujilinda na mashambulizi ya anga pamoja na kujizuia kutuma picha cha uharibifu uliofanywa na mashambulizi hayo.
Kwengineko, vikosi vya Urusi vinajaribu kuuzingira mji muhimu wa Lysychansk ulio katika mkoa wa Luhansk mashariki mwa Ukraine. Inaarifiwa vikosi hivyo vimeonekana pembezoni mwa njia za kuingia mjini humo huko upande wa Urusi ukisema tayari mapambano yameanza kuelekea katikati mwa mji.
Widodo ziarani Ukraine na Urusi kujaribu kumaliza vita
Wakati hayo yakijiri, rais wa Indonesia Joko Widodo ambaye pia ni mwenyekiti wa zamu wa kundi la mataifa yaliyostawi na yale yanayoinukia kiuchumi la G20 anaitembelea Ukraine leo kwa ziara inayolenga kutafuta njia za kumaliza vita.
Widodo ambaye amejitwika dhima ya kuwa mpatanishi binafsi kwenye mzozo wa Ukraine amepangiwa pia kuitembelea Urusi baadae wiki hii.
Tayari amekutana na rais Volodomyr Zelensky baada ya kuyatembelea maeneo ya mji mkuu Kyiv kujionea uharibifu wa majengo na miundombinu uliotakana na vita inayoendelea.