1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 3 wa familia moja wapatikana baada ya kupotea Kenya

17 Februari 2020

Watu watatu wa familia moja waliokuwa wametekwa nyara mwezi mmoja uliopita katika kijiji cha Myabogi maeneo ya kaunti ya Lamu eneo la Pwani ya Kenya wamepatikana hai katika eneo la Mtwapa, Kaunti ya Kilifi

https://p.dw.com/p/3XskO
Kenia Mombasa | Sombwana Athman wurde gekidnapped und später freigelassen
Picha: DW/F. Musa

Katika kikao na wanahabari mjini Mombasa, watatu hao wameeleza kwamba watu hao waliojitambulisha kama maafisa wa usalama wakati wakiwakamata, waliwafunga macho na kuwazuilia katika sehemu isiyojuilkana kwa muda wa mwezi mmoja na hawakuwahi kuwaambia sababu ya kuwakamata.

Sombwana Athman ameelezea kwamba walisafirishwa usiku na kuzuiliwa katika nyumba kila mmoja akizuiliwa katika chumba chake peke yake.

Maafisa hao waliwaeleza jamaa hao kwamba wanawahitjai kwa ajili ya kuwauliza maswali na kisha kuwaachilia lakini haikuwa hivyo.

Khalid Hashim ambaye ni mkulima anasema nyumba waliozuiliwa ilikuwa na mazingira ya kifahari na walikuwa wakiruhusiwa kufanya ibada na hata kupewa chakula lakini muda wote huo walikuwa wamefungwa kitambaa usoni isipokuwa wakati wa kula na swali waliloulizwa ni moja tu la iwapo wanajua walichoshikiwa.

Aisha Omar Bwanahadi naye pia alichukuliwa na watu hao na anaeleza kwamba walimuhoji na kusema hana hatia ila hakuwachiliwa hadi walipomaliza mwezi na kuja kuwachwa katika eneo la Mtwapa siku ya Jumamosi.

Ripoti ya pamoja ya mashirika ya kutetea haki za binadamu mapema mwaka huu ilionesha kuwa kiasi cha watu 43 walitekwa nyara na maafisa wa polisi mwaka jana baadhi walipatikana wamefariki na wengine hawajulikani waliko hadi sasa.

Mwandishi: Faiz Musa, DW/Mombasa