1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBurkina Faso

Watu kadhaa wameuawa katika mashambulizi mapya Burkina Faso

5 Machi 2024

Shirika la utangazaji la Ufaransa RFI, limesema watu kadhaa wameuwawa na wanamgambo wasiojulikana katika mashambulizi mapya Mashariki mwa Burkina Faso, ikiwa ni muendelezo wa mashambulizi dhidi ya raia nchini humo.

https://p.dw.com/p/4dBIT
Mauaji Burkina Faso FR
Makundi ya wanamgambo na vikosi vya serikali zinashutumiwa kwa mauaji ya raia Burkina Faso

Shirika hilo la utangazaji la Ufaransa limesema, mikanda ya vidio iliyokusanywa na waandishi wake imeonyesha miili kadhaa ya wanaume, wanawake na watoto ikiwa imetapakaa sakafuni. Vidio hizo pia ziliwaonyesha wanaume waliokuwa wamejihami wakiwa katika pikipiki wakiwachukua watoto na kuwapa kitu cha kunywa, watoto ambao wanaaminika kuwa manusura wa mkasa huo.

RFI imesema kutokana na mauaji yaliyofanyika awali ni vigumu kujua hasa iwapo waliotekeleza uovu huo ni makundi ya watu waliojihami au jeshi lenyewe la Burkina Faso. Shirika hilo halikutoa idadi kamili ya watu waliouwawa au siku mashambulizi hayo yalipofanywa kwa vijiji viwili Mashariki kwa mkoa wa Komondjari ulioko mpakani mwa Niger.

Watu kadhaa wauawa msikitini wakati wa sala ya asubuhi mashariki mwa Burkina Faso

Hadi sasa serikali ya Burkina Faso haijasema lolote juu ya ripoti ya RFI. Mwendesha mashitaka mmoja nchini humo, alisema bado wanachunguza mauaji ya watu 170 waliouwawa pale vijiji vitatu viliposhambuliwa Kaskazini mwa mkoa wa Yatenga, mnamo Februari 25.

Vikosi vya serikali pamoja na wanamgambo wamekuwa wakishutumiwa kutekeleza mauaji dhidi ya raia tangu mwaka 2015. Kwa mujibu wa kamati ya kimataifa ya uokoaji, serikali imepoteza nguvu na udhibiti wake katika karibu nusu ya taifa hilo na kuangukia mikononi mwa wanamgambo tangu mwaka 2022.

Schulze aitembelea Burkina Faso kufanya mazungumzo ya kisiasa

Svenja Schulze
Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Svenja SchulzePicha: Janine Schmitz/photothek/IMAGO

Haya yanajiri wakati Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze akianza ziara barani Afrika akiitembelea Burkina Fao na Benin kwa mazungumzo ya kisasa. Shulze ameonya kuwa ugaidi na malengo ya Urusi kutaka kuwa na ushawishi zaidi  kunatishia amani ya ukanda wa Sahel katika eneo la kusini mwa jangwa la sahara.

Svenja Schulze amekuwa waziri wa kwanza barani Ulaya kuiziuru Burkina Faso tangu yalipotokea mapinduzi ya kijeshi mwezi September mwaka 2022 yaliyompa nafasi Ibrahim Traoré kuwa kiongozi wa taifa hilo.

Schulze ni mwenyekiti wa muungano wa Sahel ulioundwa na Ujerumani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya ili kuyasaidia mataifa ya ukanda huo wa Sahel, na Ujerumani pia ndio mfadhili wa nne mkubwa wa muungano huo.

Waziri wa maendeleo wa Ujerumani kufanya mazungumzo na ECOWAS

Kwa sasa serikali ya Traore imeahirisha uchaguzi mkuu uliotarajiwa kufanyika mwaka huu na kutokana na ukosefu wa usalama nchini Burkina Faso watu zaidi ya milioni 2 wanakadiriwa kupoteza makaazi yao. Kama ilivyo kwa jirani zake Mali na Niger zinazotawaliwa kijeshi, Burkina Faso inaendelea kujisogeza zaidi kwa Urusi na kuachana na Ufaransa iliyozitawala nchi hizo wakati wa ukoloni na ambaye imekuwa ikitoa msaada wa kijeshi ili kupambana na ugaidi unaoongezeka huko.

dpa