Waziri Mkuu wa Bangladesh ajiuzulu, akimbia nchi
5 Agosti 2024Awali raia wenye hasira walikataa kutii amri ya kutotoka nje iliyotangazwa na jeshi, na kuingia mitaani kumtaka waziri mkuu huyo kujiuzulu, ambaye sasa anasemekana kukimbilia nchini India.
Wachambuzi walikuwa wanahofia kuwa ghasia za leo zingeliweza kuwa kubwa kuliko zilizoshuhudiwa siku ya Jumapili baada ya waandamanaji kukabiliana na wafuasi wanaoiunga mkono serikali, ambapo takribani watu 100 waliuawa wakiwemo maafisa 14 wa polisi.
Soma zaidi: Takribani watu 100 wameuawa katika maandamano Bangladesh
Maandamano ya wanafunzi yaliyoanza mwezi uliopita wakitaka kusitishwa kwa mfumo wa ajira serikalini wanaodai ulikuwa na upendeleo, yalishika kasi na kugeuka kuwa machafuko mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika utawala wa miaka 15 wa Sheikh Hasina.
Mtandao wa intaneti ulizimwa, ofisi za serikali na zaidi ya viwanda 3,500 vya nguo vimefungwa nchini humo.