Waziri wa ndani wa Ufaransa kujadili kuhusu uhamiaji Italia
18 Septemba 2023Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Gerald Darmanin, amesema atafanya ziara mjini Roma leo Jumatatu na kujadili na mwenzake, Matteo Piantedosi, kuhusu suala la uhamiaji, baada ya idadi kubwa ya waomba hifadhi kuwasili wiki iliyopita katika kisiwa cha Italia cha Lampedusa.
Darmanin amesema Ufaransa inalenga kuisaidia Italia kulinda mipaka yake ikiwa ni moja ya nchi za Umoja wa Ulaya zinazoshuhudia idadi kubwa ya wahamiaji wanaoingia barani humo kutoka Afrika Kaskazini. Wiki iliyopita, takriban wahamiaji 8,500 waliwasili katika kisiwa cha Lampedusa.
Ujio huu mpya wa maelfu ya wahamiaji umeibua mjadala katika mataifa ya Ulaya kuhusu sera ya pamoja ya mapokezi na kugawana wahamiaji hao.
Wiki iliyopita, Ujerumani ilichukuwa hatua ya kutowapokea wahamiaji kutokea Italia.
Jana Jumapili, Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen alitembelea visiwa hivyo na kutangaza mpango wa hatua za dharura.