Xi akutana na Macron, von der Leyen
6 Mei 2024Katika hotuba yake ya makaribisho asubuhi ya Jumatatu (Mei 6) Macron alisema ni muhimu kwa China na Ulaya kushirikiana kwenye suala la Ukraine na pia kuwa na ushindani wa haki kwenye biashara ulimwenguni.
Rais huyo wa Ufaransa Macron aliongeza kuwa yeye na Rais Xi wangeuzungumzia pia mgogoro wa Mashariki ya Kati.
Kwa upande wake, Rais Xi alisema China "inaipa kipaumbele Ulaya kwenye sera yake ya mambo ya kigeni na inauchukulia uhusiano baina ya pande hizo mbili kuwa wa kimkakati na wa muda mrefu".
Soma zaidi: Rais Xi Jinping akubali kuzungumza na Zelensky
Rais huyo wa China alitowa wito kwamba lazima wote wajitolee kuuimarisha uhusiano huo.
Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa ushindani wa haki kwenye biashara duniani, hoja ambayo aliibua pia mara ya mwisho alipokutana na Rais Xi, akisema kwamba "hali ya sasa ya ukosefu wa mizania kwenye fursa za masoko si jambo endelevu na lazima litatuliwe."
Suala la Ukraine
Katika makala yake iliyochapishwa kwenye gazeti la Le Figaro, Xi alisema anataka kushirikiana na jumuiya ya kimataifa ili kuutatua mzozo nchini Ukraine, huku akisisitiza kuwa nchi yake si sehemu wala mshirika wa vita hivyo.
Awali, Macron alikuwa amesema angelitumia fursa hii kumuonya waziwazi mgeni wake huyo juu ya hatari ya kuiunga mkono Urusi.
Mataifa ya Magharibi yamekuwa yakionesha wasiwasi baada ya mafungamano ya Beijing na Moscow kuimarika zaidi baada ya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, ambapo yanadai tayari Urusi inatumia vifaa vya China kwenye utengenezaji wa silaha.
Soma zaidi: Xi Jinping aonya dhidi ya kuanzisha Vita vipya Baridi
Kwa upande mwengie, kupokelewa rasmi kwa Rais Xi mjini Paris kuliwakera wanaharakati haki za binaadamu, wanaoutuhumu utawala wake kwa kukandamiza haki za makundi mbalimbali, wakiwemo Waislamu wa jamii ya Uighur katika jimbo la kaskazini la Xijiang, Watibeti na waandishi wa habari.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Waandishi wa Habari Wasiokuwa na Mipaka, RSF, Thibaut Bruttin, alisema Xi hastahili kupokelewa kwa heshima ya taifa.
"Rais Xi yupo Paris sasa na tunadhani kwamba kama nchi, huyu si rais wa kupokelewa kama mgeni wa heshima kama wageni wengine. Huyu ni mkandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari na ana dhama kwa kuwafunga waandishi wa habari 119, ndani ya China Bara na ndani ya Hong Kong."
Vyanzo: dpa, Reuters, AFP