Xi Jinping atoa mwito wa kujiimarisha zaidi kijeshi
16 Oktoba 2022Rais wa China Xi Jinping ametoa mwito huo huku chama tawala nchini humo cha Kikomunisti kikizidi kuimarisha udhibiti wake kwenye jamii na uchumi wa taifa hilo.
Xi Jinping ambaye katika kipindi cha miongo kadhaa amekuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa nchini China amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa chama tawala nchini humo cha Kikomunisti ambao umefuatiliwa kwa karibu na wakuu wa serikali, makampuni na umma wa China.
Soma Zaidi:Namna Xi Jinping alivyojilimbikizia madaraka katika muongo mmoja
Mkutano huo unafanyika wakati taifa hilo la pili kwa uchumi ulimwenguni likiwa linakabiliwa na hali mbaya pamoja na mivutano juu ya biashara, teknolojia na usalama si tu baina yake na Marekani bali pia majirani zake wa Asia.
Chama hicho cha Kikomunisti kinaandaa mikakati ya kuunda jamii yenye ustawi ifikapo katikati ya muongo na kuirejesha China kwenye jukumu lake la kihistoria kama kiongozi kwenye masuala ya uchumi, siasa na utamaduni.
Beijing imezidi kujimarisha uwepo wake nje ya mipaka ikiwa ni pamoja na kuanzisha mpango mpana wa barabara unaogharimu mabilioni ya dola, kujenga bandari na miundombinu mingine kote katika eneo la Asia na Afrika, lakini wachumi wanaonya kwamba mabadiliko ya kisera kwenye mfumo wake wa masoko huenda yakaathiri ukuaji wa uchumi.
Kwenye mkutano huo mkuu, kutafanyika pia mchakato wa kuwachagua viongozi watakaohudumu katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Xi, 69, anatarajiwa kuvunja mchakato wa kiutamaduni kwa kujipatia awamu ya tatu ya uongozi itakayodumu kwa miaka mitano pia pamoja na kuwapandisha vyeo washirika wake wanaounga mkono fikra zake za kuimarisha udhibiti wa chama hicho.
Soma Zaidi:China yaadhimisha miaka 70 ya utawala wa Kikomunisti
China ambayo pia ni ya pili kwa ukubwa wa bajeti ya kijeshi baada ya Marekani, kwa sasa inajaribu kuliimarisha zaidi jeshi lake kwa kutengeneza makombora, ndege za kijeshi na kuwa na kamandi nje ya taifa hilo. "Tutaongeza kasi katika kuboresha nadharia ya kijeshi, watumishi na silaha,'' alisema Xi alisema katika hotuba yake ambayo ilitatizwa na makofi kila baada ya muda mfupi. "Tutaimarisha uwezo wa kimikakati jeshini" aliongeza.
China inakabiliwa na ukosoaji wa ukiukaji wa haki za binaadamu.
Serikali ya Xi, katika utawala wake wa muongo mmoja imejaribu kutekeleza sera ngumu ya mambo ya kigeni, huku ikiimarisha udhibiti dhidi ya uhuru wa kujieleza na hata upinzani nchini China.
Serikali yake aidha inakabiliwa na ukosoaji mkali dhidi ya madai kuhusiana na kuwatia watu vizuizini kiholela pamoja na ukandamizaji mwingine dhidi ya jamii ya walio wachache ya Waislamu lakini pia kuwatfunga jela wakosoaji wa serikali.
Shirika la kimataifa la utetezi wa haki za binaadamu la Amnesty International limeonya leo hii kwamba iwapo Xi ataongezewa muda mamlakani itakuwa "ni balaa kubwa kwenye eneo la haki za binaadamu".
China yasema suala la Taiwan, ni jukumu lake.
Kuhusiana na mvutano kati yake na Taiwan, Xi amesema hilo ni suala la China, na ni jukumu lao kusuluhisha mzozo baina yao. China na Taiwan walitengana nwaka 1949 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Beijing hivi karibuni imeimarisha hatua zake za kuidhibiti Taiwan kwa kurusha ndege za kivita na mabomu karibu na kisiwa hicho, na hasa baada ya ziara ya spika wa bunge la Marekani, Nancy Pelosi huko Taiwan mwezi Agosti.
Mwaka 2018 Xi Jinping aliweka wazi nia yake ya kuaka kuondolewa kwa kipengele cha awamu mbili za urais kwenye katiba ya China. Maafisa wanasema hatua hiyo itamfanya Xi kusalia mamlakani na kufanya mageuzi. Aidha chama hicho kinatarajiwa kuifanyia mabadiliko katiba yake, ili kuongeza hadhi ya uongozi wa Xi baada ya kuongeza itikadi yake binafsi ya Wazo la Xi Jinping ama "Xi Jinping Thought" mnamo mwaka 2017.
Soma Zaidi;Itikadi za Xi Jinping zapongezwa
Msemaji wa mkutano huo Sun Yeli amesema jana Jumamosi kwamba mabadiliko hayo huenda yakaendana na mahitaji mapya ya kuimarisha maendeleo ya chama hicho, ingawa hakutoa ufafanuzi zaidi.
Mashirika: AP