Zelensky awashukuru wanaopinga uvamizi
17 Agosti 2022Akizungumza usiku wa kuamkia Jumatano, saa chache baada ya kambi ya kijeshi katika eneo linalokaliwa kimabavu na Urusi la Crimea kushambuliwa kwa miripuko kadhaa, Zelensky amesema chanzo cha miripuko hiyo inaweza kuwa na sababu mbalimbali ikiwemo uzembe.
"Kila siku tunasikia taarifa kuhusu miripuko katika eneo linalokaliwa na wavamizi. Ninawaomba watu wa Crimea na majimbo mengine ya kusini mwa nchi ambayo pia yanakaliwa, Donbas na Kharkiv kuwa makini sana," alifafanua Zelensky.
Zelensky amewatolea wito wananchi wa Ukraine kutozisogelea kambi za kijeshi zinazodhibitiwa na jeshi la Urusi na maeneo yote ambayo jeshi hilo linahifadhi silaha, vilipuzi na vifaa vingine vya kijeshi.
Nayo wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa hujuma ndiyo chanzo cha miripuko hiyo katika ghala la jeshi kwenye jimbo la Dzhankoy huko Crimea.
Ukraine haijathibitisha rasmi kama inahusika na miripuko hiyo, lakini iwapo vikosi vya Ukraine vinahusika, inaonesha kuwa inaweza kufanya operesheni za siri dhidi ya adui yake.
Guterres kwenda Ukraine na Uturuki
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatarajiwa kuizuru Ukraine siku ya Alhamisi kwa ajili ya kukutana na Zelensky pamoja na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.
Viongozi hao wanatarajiwa kujadiliana kuhusu mkataba wa nafaka unaoiruhusu Ukraine kusafirisha chakula kwenda katika masoko ya dunia ili kusaidia kuupunguza mzozo wa njaa ulimwenguni. Mkataba huo unasimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema umuhimu wa kupatikana suluhisho la kisiasa katika vita, pia litaibuliwa wakati wa mkutano huo utakaofanyika katika mji wa Lviv ulioko magharibi mwa Ukraine.
Kwa mujibu wa Dujarric, viongozi hao watatu pia watajadiliana hali katika kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia kinachodhibitiwa na Urusi, ambako Urusi na Ukraine zimetupiana lawama za kushambuliana kwa makombora.
Siku ya Ijumaa Guterres ataizuru Odesa ambayo ni mojawapo ya bandari tatu zinazotumika kusafirisha nafaka.
Jumamosi ataelekea Uturuki ambapo atakitembelea kituo cha Istanbul kinachoratibu usafiri wa meli katika Bahari Nyeusi ambacho kinajumuisha makubaliano ya pande nne yanayozihusisha nchi za Ukraine, Urusi, Uturuki na Umoja wa Mataifa.
Ama kwa upande mwingine, kampuni kubwa ya Ujerumani ya kusafirisha gesi ya Uniper imepata hasara ya zaidi ya euro bilioni 12 katika nusu ya kwanza ya mwaka, ikiwa ni zaidi ya nusu iliyokuwa imekadiriwa kuhusiana na mzozo wa gesi na Urusi. Kampuni hiyo imesema Jumatano kuwa kiasi cha euro bilioni 6.5 kinahusishwa na kukatizwa kwa usambazaji wa gesi kutoka Urusi kama matokeo ya vita vya Ukraine.
(AFP, DPA, AP, Reuters)