Zimbabwe yashinikiza biashara halali ya pembe za ndovu
25 Mei 2022Wahusika wametahadharisha iwapo nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika haitaruhusiwa kuuza tani zipatazo 130 za pembe za ndovu zinazokadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 600, basi pana uwezekano Zimbabwe ikajiondoa kutoka kwenye mkataba wa kimataifa kuhusu biashara ya bidhaa ambazo zimo hatarini kutoweka, CITES.
Mkutano huo wa siku tatu unafanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Hwange, ambayo ni mbuga kubwa ya wanyamapori iliyopo kusini magharibi mwa Zimbabwe. Wawakilishi kutoka nchi 16 za Afrika, pamoja na Japan, China na watumiaji wakuu wa pembe za ndovu, wanahudhuria mkutano huo.
Soma pia: Wanawake Zimbabwe wapambana dhidi ya ubaguzi wa kijinsia
Wiki iliyopita wajumbe kutoka baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya, Uingereza, Marekani na Canada walionyeshwa sehemu zilizowekewa ulinzi mkali katika mji wa Harare ambazo zimejaa meno ya tembo katika hatua ya kujaribu kushawishi uungwaji mkono wa kimataifa ili Zimbabwe iruhusiwe uuzaji halali wa pembe zake za ndovu.
Juhudi za serikali ya Zimbabwe za kuuza pembe hizo za ndovu zinapingwa na makundi ya wahifadhi ambayo yanasema uuzaji wowote wa pembe za ndovu utachochea ujangili wa uwindaji haramu nchini humo.
Muungano wa mashirika 50 ya watetea haki za wanyama na wanyamapori katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa siku ya Jumatatu, yamesema mkutano huo unatoa ishara ambayo inaweza kuwa ni hatari kwa sababu majangili na makundi ya wahalifu yatachukulia kuwa mnyama tembo ni sawa na bidhaa ya kawaida tu, na kwamba biashara ya pembe za ndovu inaweza kuanzishwa tena hali ambayo itaongeza kitisho kwa wanyama hao.
Mkataba wa CITES ulipiga marufuku biashara ya pembe za ndovu mnamo mwaka 1989
Nchi za Kusini mwa Afrika zimewahi kuruhusiwa mara mbili kuuza hifadhi za pembe za ndovu kwa Japan na China mnamo miaka ya 1997 na 2008 na mauzo hayo yalisababisha kupanda kwa kasi matendo ya uwindaji haramu barani Afrika, yamesema mashirika hayo.
Mashirika hayo yamesema kuhalalisha tena biashara ya meno ya tembo kunaweza kuleta matokeo mabaya kwa mara nyingine tena. Upinzani mkubwa pia unatoka nchini Kenya na kwa wanachama wengine 32 kutoka nchi za Afrika Mashariki na Afrika Magharibi nchi ambazo zina tembo wachache.
Nchi hizo zimesema kufungua upya kisheria biashara ya kimataifa ya biashara ya pembe za ndovu, hata kwa mnada wa mara moja, inaweza kusababisha kuongezeka kwa matendo ya uwindaji haramu.
Soma pia:Zimbabwe: Ni wakulima wa kigeni tu watakaorejeshewa ardhi
Mkataba wa kimataifa kuhusu biashara ya bidhaa ambazo zimo hatarini kutoweka, CITES ulipiga marufuku biashara ya kimataifa ya pembe za ndovu mnamo mwaka 1989 ili kupunguza ujangili wa uwindaji haramu.
Mbali na kupiga marufuku uuzaji wa pembe za ndovu, CITES mnamo mwaka 2019 pia iliweka vizuizi kwa uuzaji wa meno ya tembo yaliokamatwa kutoka Zimbabwe na Botswana, hatua ambayo iliwafurahisha baadhi ya wahifadhi wa wanyama pori lakini wakati huo huo maafisa wa mbuga za wanyamapori wanahangaika kusimamia mbuga zao zilizojaa Wanyama hao.
Zimbabwe imesema idadi ya tembo nchini humo inaongezeka kwa kasi kati ya asilimia 5 hadi 8 kwa mwaka, kiwango ambacho haiwezi kukimudu. Zimbabwe imesema inahitaji sana fedha kutokana na mauzo ya pembe za ndovu ili kuweza kusimamia idadi kubwa ya tembo nchini humo, ambayo imeongezeka na kufikia kiwango cha hatari.
Maafisa wa mbuga za Wanyama wanakadiria kuwa idadi maradufu ya tembo 100,000 inakiuka uwezo wa mbuga za kitaifa nchini humo na kwamba tembo hao waliojaa wanaharibu miti na vichaka ambavyo ni muhimu kwao na pia kwa wanyamapori wengine. Nchi jirani ya Botswana ina idadi kubwa ya tembo duniani, nchi hiyo ina zaidi ya tembo 130,000.
Kwa pamoja Zimbabwe na Botswana zina karibu asilimia 50 ya tembo wote duniani. Nchi hizo mbili zinajitahidi kukabiliana na idadi kubwa ya tembo inayoongezeka.
Zimbabwe na Botswana zinasema hazina vifaa vya kutosha vya kukabiliana na wawindaji haramu bila ya fedha zinazotokana na mauzo ya pembe za ndovu, hasa kwa sababu ya kupungua kwa mapato ya utalii ulioathirika pakubwa na janga la ugonjwa wa Covid-19.