1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaArmenia

Armenia na Azerbaijan kuchukua hatua za kurejesha uhusiano

8 Desemba 2023

Armenia na Azerbaijan zimekubaliana juu ya mpango wa kubadilishana wafungwa wa kivita na kushirikiana kuelekea kusaini mkataba wa amani. Umoja wa Ulaya na Marekani na uturuki zimepongeza hatua hiyo.

https://p.dw.com/p/4ZvFR
Ilham Aliyev - Nikol Pashinyan - Charles Michel
Picha: Dursun Aydemir/AA/picture alliance

Umoja wa Ulaya umesema unapongeza hatua hiyo na kuitaja kuwa muhimu sana kuelekea kwenye amani katika eneo ambalo linakabiliwa na migogoro kwa muda mrefu. Chini ya makubaliano hayo Azerbaijan imesema itawaachilia huru wanajeshi 32 wa Armenia huku Armenia ikiahidi kuwa itawaachia wanajeshi wawili wa Azerbaijan.

Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev katika Kongamano la 74 la Kimataifa la Wanaanga mjini Baku, Azerbaijan tarehe 02 Oktoba 2023.
Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev katika Kongamano la 74 la Kimataifa la Wanaanga mjini Baku, Azerbaijan tarehe 02 Oktoba 2023. Picha: Azerbaijani Presidency/AA/picture alliance

Nchi hizo mbili zimesema katika taarifa ya pamoja kwamba zinaamini kuwa ipo nafasi ya kihistoria ya kufikia amani iliyosubiriwa kwa muda mrefu. Nchi hizo mbili zimesema zinakusudia kurekebisha uhusiano kati yao na kufikia makubaliano ya amani katika mkataba utakaozingatia misingi ya heshima kulingana na kanuni za uhuru na uadilifu wa kikanda.

Hadi tamko hilo la leo Ijumaa, nchi hizo mbili zilikuwa zinazozana vikali kuhusu mchakato wa amani na kulikuweko na hali ya kutoaminiana.

Soma:Armenia na Azerbaijan zakubaliana msingi wa mkataba wa amani

Vilevile nchi hizo hazikukubaliana kuhusu nchi gani katika eneo la Ulaya mashariki itakayokuwa mwenyeji wa mkutano wa hali ya hewa mwaka ujao wa 2024. Lakini sasa zimefikia maelewano na katika sehemu ya makubaliano hayo, Armenia imekubali kuondoa pingamizi yake juu ya Azerbaijan kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa wa mwaka ujao kuhusu mabadiliko hali ya hewa.

Rais wa Armenia Vahagn Khachaturyan alipohudhuria sherehe za kuapishwa kwake huko Yerevan mnamo Machi 13, 2022.
Rais wa Armenia Vahagn Khachaturyan alipohudhuria sherehe za kuapishwa kwake huko Yerevan mnamo Machi 13, 2022.Picha: KAREN MINASYAN/AFP/Getty Images

Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel amepongeza na kusifu makubaliano hayo kuwa ni ya mafanikio makubwa. Michel pia amesema ameukaribisha mpango wa kuwaachilia wafungwa na hivyo kuashiria nafasi kubwa ya mwanzo ambao haujawahi kutokea wa mazungumzo ya kisiasa kati ya pande hizo mbili. Michel ametoa wito kwa Armenia na Azerbaijan kukamilisha makubaliano ya amani haraka iwezekanavyo. 

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya alipoongea na waandishi wa habari siku ya mwisho ya mkutano huo, katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Oktoba 27, 2023.
Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya alipoongea na waandishi wa habari siku ya mwisho ya mkutano huo, katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Oktoba 27, 2023.Picha: Kenzo Tribouillard/AFP/Getty Images

Marekani pia imeukaribisha mpango huo, ikisema kubadilishana kwa wafungwa wa kijeshi ni  hatua muhimu inayojenga ujasiri wakati pande zhizo mbili zikiendelea kukamilisha hatua za kufikiwa makubaliano ya amani na kurejesha uhusiano wa kawaida kati yao.

Uturuki pia imepongeza makubaliano kati ya mahasimu wakubwa Armenia na Azerbaijan hatua ya kubadilishana wafungwa wa kivita na kufanya kazi katika kurejesha uhusiano uliovunjika miongo kadhaa kutokana na mzozo katika eneo la Nagorno-Karabakh.

Vyanzo:AP/RTRE/AFP