1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miito ya kusitisha mapigano Gaza yazidi kuongezeka

18 Desemba 2023

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litapiga kura juu ya rasimu mpya ya kutaka kusimamishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza. Marekani kwa upande wake imeongeza kuonyesha kutokuwa na subira na mshirika wake mkuu Israel

https://p.dw.com/p/4aJ0a
USA, New York | Tagung des UN-Sicherheitsrats
Picha: Yuki Iwamura/AFP/Getty Images

Rasimu hiyo mpya, iliyopendekezwa na Umoja wa Falme za Kiarabu inataka kusitishwa kwa haraka vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza ili kuruhusu kuwepo njia salama za kufikisha misaada ya kibinaadamu katika eneo hilo.

Rasimu hiyo mpya pia inathibitisha kuunga mkono suluhisho la mataifa mawili na inasisitiza umuhimu wa kuunganisha Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi chini ya Mamlaka ya Palestina.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Gaza, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York mnamo Desemba 8, 2023.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Gaza, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York mnamo Desemba 8, 2023.Picha: YUKI IWAMURA/AFP

Hatua hiyo imekosolewa na Israel na Marekani, ambazo zimesema rasimu hiyo hailitaji kundi la Hamas, ingawa inataka kuachiliwa mara moja na bila masharti mateka wote na inalaani mashambulio yote yanayowalenga raia.

Soma Pia:Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin azuru Israel kujadili vita vyake Gaza. 

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin akiwa nchini Israel anatarajiwa kuishinikiza nchi hiyo kusitisha operesheni yake ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza.

Ziara hiyo ya Austin ni mtihani mwingine kwa Marekani kama itafanikiwa katika kuwaondolea madhila raia wa Palestina kutokana na vita vya mshirika wake ambaye Marekani inamuunga mkono na kusisitiza kuwa haitabadili msimamo wake kwamba Israel inayo haki ya kujilinda kwa kuzingatia misingi ya kimataifa y  a kibinaadamu. 

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin wakati wa mkutano na waandishi wa habari , Oktoba 13, 2023 huko Tel Aviv, Israel.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin wakati wa mkutano na waandishi wa habari , Oktoba 13, 2023 huko Tel Aviv, Israel.Picha: Chad Mcneeley/Dod/picture alliance

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na Mwenyekiti wa Majenerali wa Kijeshi wa Marekani, CQ Brown, wamewasili mjini Tel Aviv hii leo, na wanatarajiwa kuwashinikiza viongozi wa Israel waingie kwenye awamu mpya ya vita vyake dhidi ya kundi la Hamas baada ya wiki kadhaa za mashambulizi makubwa ya mabomu na operesheni ya ardhini.

Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, washirika wa karibu wa Israel, wanaunga mkono wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano mwishoni, huku waandamanaji nchini Israel wakiitaka serikali yao ianzishe upya mazungumzo na Hamas juu ya kuwaachilia mateka zaidi baada ya mateka watatu raia wa Israel kuuawa kimakosa na jeshi la nchi hiyo licha ya kwamba walipeperusha bendera nyeupe.

Som Pia:Israel yaendeleza mashambulizi Gaza huku miito ya usitishwaji vita ikitolewa

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea kupigana hadi itakapowaondoa Hamas madarakani, kuharibu kabisa uwezo wa kijeshi wa kundi hilo na kuwarudisha nyumbani mateka kadhaa ambao bado wanashikiliwa na kundi hilo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipohudhuria mkutano wa kila wiki wa baraza la mawaziri katika ofisi ya Waziri Mkuu mjini Jerusalem, Jumapili, Desemba 10, 2023
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipohudhuria mkutano wa kila wiki wa baraza la mawaziri katika ofisi ya Waziri Mkuu mjini Jerusalem, Jumapili, Desemba 10, 2023Picha: Ronen Zvulun/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita vya Gaza mnamo Oktoba 7, meli iliyobeba misaada iko njiani kutoka Cyprus kuelekea eneo la Palestina. Meli hiyo ya jeshi la wanamaji la Uingereza imebeba takriban tani 80 za msaada. Usafirishaji wa shehena hiyo umepangwa kwa ridhaa ya Israel na Misri.

Vyanzo:  AFP/DPA