Marekani na Israel kujadili operesheni ya kijeshi Gaza
18 Desemba 2023Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin atazuru Israel leo Jumatatu kama sehemu ya safari yake katika eneo la Mashariki ya Kati ambapo pia atakwenda Bahrain na Qatar. Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema Austin atakutana na viongozi wa kijeshi wa Israel hususan kusisitiza ahadi thabiti ya Marekani ya kuunga mkono haki ya Israel ya kujilinda kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani pia atazungumzia hatua ambazo Israel inachukua kwa ajili ya kuepuka madhara ya raia pamoja na mipango ya Israel kwa Gaza baada ya kumalizika mapigano. Ziara ya Austin nchini Israel inafanyika wakati ambapo mataifa mengi ya Magharibi yanaishinikiza nchi hiyo kusitisha mapigano.
Soma Pia: Papa Francis aomboleza kifo cha "raia wasio na ulinzi" ukanda wa Gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Catherine Colonna hapo jana Jumapili alitoa wito wa kufikiwa suluhisho la haraka ili liwe njia ya kuachiliwa kwa mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas amesema pia litawezesha kupelekwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, na kuwa ndio mwanzo wa kuelekea kupatikana suluhisho la kisiasa kati ya Israel na Wapalestina. Ujerumani na Uingereza kwa upande wao, zimetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kupiga kura hii leo Jumatatu kuhusu azimio jipya la kutaka kusitishwa mapigano huko Gaza na kwamba Israel na Hamas ziruhusu shughuli za kupelekwa misaada katika Ukanda wa Gaza kupitia njia za ardhini, baharini na angani zitakazosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Soma Pia:Jeshi la Israel limegundua handaki kubwa zaidi linalotumiwa na Hamas
Wakati huo huo Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema limegundua handaki kubwa la kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza. IDF imesema mfumo huo una urefu wa mita 400 kutoka kwenye kivuko cha mpaka cha Erez kati ya Israeli na eneo la pwani ya Gaza.
Huku hayo yakiendelea katika mzozo wa Israel na wapiganaji wa Hamas mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema WHO imesikitishwa na uharibifu mkubwa katika Hospitali ya Kamal Adwan iliyopo kaskazini mwa Gaza baada ya kituo hicho kuvamiwa na wanajeshi wa Israel katika siku kadhaa zilizopita. Amesema hospitali hiyo imeshindwa kufanya kazi na hivyo kusababisha vifo vya wagonjwa wanane.
Hata hivyo Mwakilishi wa Israel katika Umoja wa Mataifa amesema katika tamko lake Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus hakutaja juu ya kujificha kwa wapiganaji Hamas katika hospitali hiyo.
Soma Pia:Mwanadiplomasia wa Ufaransa ataka kusitishwa mapigano Gaza
Jeshi la Israel awali lilisema lilipata silaha na liliwakamata karibu wapiganaji 80 wa Hamas katika hospitali hiyo. Marekani, Umoja wa Ulaya, Ujerumani na nchi nyingine zimeiainisha Hamas kama kundi la kigaidi.
Vyanzo: DW Page/DPA/RTRE/AFP