1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden na Harris wafanya kampeni kwa pamoja

Josephat Charo
3 Septemba 2024

Rais wa Marekani Joe Biden na makamu wake Kamala Harris wamefanya kampeni ya pamoja kwa mara ya kwanza huko Pennsylvania tangu Biden alipojiondoa kuwania urais wa Marekani.

https://p.dw.com/p/4kCYg
Rais wa Marekani, Joe Biden, kushoto, na Kamala Harris
Rais wa Marekani, Joe Biden, kushoto, na Kamala HarrisPicha: Elizabeth Frantz/REUTERS

Rais wa Marekani Joe Biden na makamu wake Kamala Harris wamefanya kampeni pamoja kwa mara ya kwanza jana Jumatatu katika tukio la hadharani linaloonesha umoja tangu Harris alipochukua nafasi ya Biden kama mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa Novemba 5.

Viongozi hao wawili wamehudhuria hafla ya kuadhimisha siku ya wafanyakazi Marekani pamoja na wanachama wa shirikisho katika jimbo lenye ushindani mkali katika uchaguzi la Pennsylvania.

Kabla hafla ya pamoja na Biden huko Pittsburgh, Pennsylvania, Harris aliuhutubia umati wa watu mjini Detroit, jimboni Michigan, akitafuta kuimarisha uungwaji mkono wa vyama vya wafanyakazi na wapigaji kura wa tabaka la wafanyakazi ambao mgombea wa chama cha Republican Donald Trump anadai ni ngome yake.

Biden, mwenye umri wa miaka 81, alijiondoa kutoka kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais mwishoni mwa mwezi Julai chini ya shinikizo kubwa lililokuwa likiongeza, kufuatia kufanya vibaya katika mdahalo dhidi ya Donald Trump.

Hatua yake ya haraka kumuidhinisha na kumuunga mkono makamu wake Kamala Harris, mwenye umri wa miaka 59, kulimsaidia kupata uungwaji mkono wa chama cha Democratic na kuteuliwa rasmi kama mgombea wiki chache baadaye.