Biden: Palestina tumieni siasa kupata amani ni Israel
15 Julai 2022Rais Joe Biden wa Marekani ameyasema hayo alipokutana na kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas mapema leo kabla ya kuelekea Saudi Arabia.
Biden ambaye kwa mara ya kwanza anazuru maeneo ya Palestina akiwa rais, ametumia ziara yake kuthibitisha kwa mara nyingine juu ya juhudi kamili za Marekani katika kuhakikisha muuaji wa mwandishi wa habari wa televisheni ya Al-Jazeera, mwenye asili ya Palestina na Marekani, Shireen Abuh Akleh anapatikana na kuwajibishwa.
Biden ambaye pia amesisitiza mara kwa mara kuhusu Marekani inavyounga mkono Palestina kutambulika kama taifa tangu alipoianza ziara yake ya Mashariki ya Kati siku ya Jumatano amekiri waziwazi kwamba lengo la suluhu ya mataifa mawili ni sawa na ndoto za alinacha, katika mchakato mzima wa kusaka amani kati ya Israel na Palestina.
"Hatutaukatia tamaa mchakato wa kutafuta amani. Ni lazima kuwepo na upeo wa kisiasa ambao watu wa Palestina wanaweza kuuona ama angalau kuuhisi. Hatutaruhusu hali ya kukosekana kwa matumaini ituvurugie mustakabli wetu." alisema Biden.
Alitoa matamshi hayo akiwa Bethlehem, katika eneo linalokaliwa kimabavu na Israel kwenye Ukingo wa Magharibi.
Rais Mahmud Abbas hakutofautiana na Biden kuhusiana na suala hilo la suluhu ya mataifa mawili, akisema kuna uwezakano hafifu mno wa njia hiyo kutumika ili kupata amani kati yao na Israel. Amesema fursa ya suluhu ya mataifa mawili katika mzozo wa mipaka wa tangu mwaka 1967 inaweza ikapatikana leo, lakini haiwezi kudumu kwa muda mrefu.
Alizungumzia pia ghadhabu ya muda mrefu ya watu wa Palestina dhidi ya uvamizi huo wa Israel uliodumu kwa miaka mitano sasa. Kiongozi huyo alisema Wapalestina wana matumaini na juhudi za Marekani za kuzuia makazi na machafuko baina ya walowezi, lakini pia kumaliza hatua za Wapalestina kuondolewa kwenye ardhi yao. Akasisitiza kwamba mambo haya yote ni lazima yaanze na Palestina kutambuliwa kama taifa.
Mahmud pia amezungumzia mauaji ya mwandishi wa habari Abu Akleh, ambaye aliuawa akiwa kazini kwenye mji wa Jenin, ulioko kwenye eneo hilo la Ukingo wa Magharibi mwezi Mei, na kuiomba Marekani kuwaunga mkono katika juhudi zao za kuwawajibisha wahusika wa mauaji hayo.
Tizama Video:
Rais Biden ameondoka Tel Aviv akiwa kwenye safari ya kihistoria ya moja kwa moja kutoka Israel hadi Saudi Arabia, ikiwa ndio kituo chake cha mwisho katika ziara yake ya kwanza ya Mashariki ya Kati akiwa rais.
Mashirika: AFPE/RTRE