1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Blinken kufanya mazungumzo na Rais wa Palestina

10 Januari 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken anatarajiwa hii leo kufanya mazungumzo na Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas.

https://p.dw.com/p/4b3EL
Eneo Huru la Palestina | Ziara ya Antony Blinken huko Ramallah
Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas(kulia) akipeana mkono na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken kabla ya mkutano wao huko Muqata, katika mji wa Ramallah, ambako kuna makazi ya rais Picha: Saul Loeb/AP Photo/picture alliance

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Marekani yuko ziarani katika eneo la Mashariki ya Kati, hii ikiwa ni mara ya nne tangu vita hivyo vilipoanza na jana alikutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Blinken ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba Marekani itaendelea kumuunga mkono kama mshirika wake, lakini pia ikatoa wito wa hatua zaidi za kuwalinda raia waliokwama katika eneo hilo la Palestina lililozingiwa na kuongeza kuwa idadi ya watu wanaoathirika kila siku na vita hivyo huko Ukanda wa Gaza na hasa wanawake na watoto ni kubwa mno.

Majaribio kadhaa ya kusaka suluhu yameshindwa, lakini kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh wiki iliyopita aliashiria kuliunga mkono pendekezo la utawala mmoja wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Soma pia: Israel yatakiwa kupunguza mashambulizi yake Gaza 

Taarifa kutoka kwenye kasri la mfalme wa Jordan imesema, Mfalme Abdullah II atakutana na Abbas na Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sissi hii leo kujadiliana kuhusu Gaza, lakini pia juhudi za kushinikiza usitishwaji wa haraka wa mapigano kwenye eneo hilo.

Mapema, Blinken aliiambia Israel kwamba italazimika kufanya maamuzi magumu ikiwa inataka kurekebisha mahusiano na majirani zake na kuwaunga mkono viongozi wa Palestina wanaoonyesha nia ya kupata suluhu.

Israel Tel Aviv | Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwasili Tel Aviv wakati wa ziara yake ya wiki moja inayolenga kutuliza hali katika ukanda wa Mashariki ya Kati, Januari 8, 2024Picha: Evelyn Hockstein/Pool/AP/picture alliance

Blinken, tayari ameyatembelea mataifa ya Kiarabu yanayopaka na Israel katika siku za karibuni kujadiliana juu ya mikakati ya siku za usoni ya kiutawala kwenye Ukanda wa Gaza. Marekani na Israel wanasimama pamoja katika vita dhidi ya Hamas, ambalo wanalitaja kama kundi la kigaidi, lakini wakipishana kuhusiana na mustakabili wa Gaza.

Vikosi vya Israel vyaendeleza mashambulizi, WHO yalia juu ya hali mbaya

Taarifa kutoka Tel Aviv zinasema vikosi vya Israel vimeendeleza mashambulizi katika jiji la Khan Younis na katika kambi ya wakimbizi ya al-Maghazi iliyoko katikati mwa Ukanda wa Gaza. Wanajeshi hao wameyalenga pia maeneo 150 ya Hamas kwa siku moja, hii ikiwa ni kulingana na jeshi hilo, IDF, mapema leo. 

Mashambulizi hayo yanaendelea huku Shirika la Kimataifa la Afya - WHO- jana Jumanne likisema hali ya kiafya na mzozo wa kibinaadamu umezidi kuongezeka katika wiki za karibuni kwenye eneo hilo na kutoa wito wa kufunguliwa njia za kupitisha misaada zaidi ya kiutu ili kupelekwa misaada ya dharura.

Mratibu wa huduma za tiba za dharura wa shirika hilo Sean Casey akiwa huko Rafah, "Hapa Rafah nilipo watu wanalala kila mahali. Wengine wanalala chini ya maturubai, chini ya mahema ya muda, na pia katika makazi yaliyofurika watu.”

Aidha, Israel imesema imemuua kamanda wa kikosi cha droni cha Hezbollah, ingawa kundi hilo la wanamgambo limeyapuuza madai hayo. Msemaji wa IDF kwa lugha ya Kiarabu Avichay Adraee amesema wamemuua Ali Hussein Barji, aliyeongoza operesheni kadhaa kwa kutumia droni za kushambulia pamoja na droni za ujasusi dhidi ya Israel na IDF.