Netanyahu awataka wanachama wa Hamas kujisalimisha haraka
11 Desemba 2023Israel imesema imeyashambulia maeneo yapatayo 250 katika Ukanda wa Gaza ikiwemo baadhi ya mifumo ya njia za chini ya ardhi. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewataka wanachama wa Hamas 'kujisalimisha haraka', Netanyahu amesema makumi ya wengine tayari wamejisalimisha kwa vikosi vya Israel.
" Katika siku chache zilizopita, makumi ya magaidi wa Hamas wamejisalimisha kwa vikosi vyetu. Wameweka silaha zao chini na kujisalimisha kwa wanajeshi wetu mashujaa. Itachukua muda zaidi, vita bado vinarindima, lakini huu ndio mwanzo wa kutokomezwa kundi la Hamas. Nawaambia magaidi wa Hamas: Imefikia tamati, msife kwa ajili ya Yahya Sinwar. Jisalimisheni sasa.”
Hamas imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na mataifa kadhaa ya Magharibi kuwa kundi la kigaidi. Inaaminika kuwa kiongozi wa kundi la Hamas Yahya Sinwar amejificha kwenye mahandaki huko Gaza. Kukamatwa kwake akiwa hai au mwili wake kupatikana akiwa amekufa ni moja ya malengo ya vikosi vya Israel katika operesheni yao ya kijeshi huko Gaza.
Soma pia: Gaza ni 'jehanamu ya dunia' - Lazzarini
Hamas wameonya kuwa hakuna mateka wa Israel atakayeondoka akiwa hai iwapo matakwa yao ya kuachiliwa kwa wafungwa Wakipalestina hayatatekelezwa.
Hali mbaya ya kibinaadamu huko Gaza
Bodi ya utendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imepitisha azimio la kutaka kupelekwa mara moja kwa misaada zaidi ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza ambao kwa sasa uko chini ya vizuizi kutoka Israel na Misri.
Muswaada wa azimio hilo , uliowasilishwa na Afghanistan, Qatar, Yemen na Morocco, uliomba kuruhusiwa kuingia katika eneo hilo kwa wahudumu wa afya pamoja na vifaa vya matibabu. WHO itatakiwa pia kufuatilia vurugu dhidi ya wahudumu wa afya na wagonjwa lakini azimio hilo linalenga pia kupatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali huko Gaza.
Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema bodi ya wanachama 34 ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imepata "azimio la kwanza la makubaliano kuhusu mzozo huo ulioanza miezi miwili iliyopita.
Soma pia: Ghebreyesus: Vita vimeudhoofisha mfumo wa afya Ukanda wa Gaza
Marekani haikupinga azimio hilo lakini imesema limekosa uwiano huku Canada ikibainisha kuwa azimio hilo halikutaja jukumu kamili la kundi la Hamas katika vita hivyo.
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina, Filippe Lazzarini, ameielezea hali katika Ukanda wa Gaza kuwa mbaya kuliko wakati wowote ule.
Kesho Jumanne, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litakutana ili kujadili mgogoro wa kibinadamu huko Gaza baada ya Marekani kuzuia wiki iliyopita azimio la Baraza la Usalama lililokuwa na lengo la kuhimiza usitishwaji mapigano huko Gaza.