1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kusini

Chama tawala chamkosoa Rais wa Korea Kusini

Saleh Mwanamilongo
6 Desemba 2024

Vyama vikuu vya kisiasa vya Korea Kusini vinafanya mazungumzo ya dharura huku wabunge wakijadili kuharakisha kura ya kumtimua Rais Yoon Suk Yeol.

https://p.dw.com/p/4npZl
Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini
Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol wa Korea KusiniPicha: AP Photo/picture alliance

Wakati wa mkutano wa chama, kiongozi wa chama tawala cha PPP, Han Dong-hun alisisitiza haja ya kusimamisha haraka majukumu ya rais Yoon Suk Yeol. Dong-Hun amesema rais alichukua hatua ya kutisha na vitendo vya hatari, katika tamko lake la kuiweka nchi hiyo chini ya amri ya kijeshi. Kiongozi huyo wa wabunge wa chama tawala amesema anazo taarifa kwamba rais aliamuru hata kukamtwa kwa viongozi wa kisiasa.

"Nilisikia kutoka kwa chanzo cha kuaminika kwamba Rais Yoon Suk Yeol aliamuru utawala wa amri ya kijeshi utakapoanza kamanda wa ujasusi awakamate  viongozi wakuu wa kisiasa, kwa  tuhuma za 'kula njama dhidi ya serikali' . Hata hivyo, rais amekataa kukubali kwamba haikuwa sahihi kutangaza sheria ya kijeshi.", alisema Dong-Hun.

"Kuna hatari kubwa ya kufanya matendo makubwa zaidi"

Kabla ya Han Dong Yun kuendelea kusema : "Kwa hivyo, ikiwa Rais Yoon Suk Yeol ataruhusiwa kuendelea na shughuli za serikali, kuna hatari kubwa ya kufanya matendo makubwa zaidi kama vile kujaribu tena kuweka sheria ya kijeshi, jambo ambalo linaweza kuiweka Jamhuri ya Korea na raia wake katika hatari kubwa."

Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini imesema imemsimasha kazi kamanda wa ujasusi, Yeo In-hyung, ambaye imedaiwa alipewa amri ya kuwaweka kizuizini wanasiasa.

Taarifa ya wizara hiyo iliendelea kusema kwamba maafisa wakuu wengine wawili, akiwemo kamanda wa kamandi maalumu wa vita, wamesimamishwa pia kazi. Mwendesha mashtaka wa Korea Kusini ametoa amri ya kutosafiri nje ya nchi kwa maafisa kadhaa wa jeshi.

Wanasiasa waliolengwa kukamtwa kufuatia amri ya rais ni pamoja ni pamoja na kiongozi wa chama tawala bungeni, kiongozi wa upinzani na Spika wa Bunge la Kitaifa. Lakini Mkurugenzi wa shirika la kijasusi alitilia shaka taarifa hizo. Akisema kwamba hakuwahi kupokea maagizo yoyote kutoka kwa rais Yoon Suk Yeolya kuwatia nguvuni wanasiasa hao.

Shinikizo la upinzani

Wafuasi wa upinzani wakiandamana mbele ya makao ya bunge ya Korea Kusini
Wafuasi wa upinzani wakiandamana mbele ya makao ya bunge ya Korea KusiniPicha: Chris Jung/NurPhoto/picture alliance

Mapema Siku ya Ijumaa, wafuasi wa upinzani walikusanyika kwenye majengo ya bunge, wakiwa na mabango wakitaka rais aondolewe madarakani.

Vyama vya upinzani vinashinikiza kura ya kutokuwa na imani na rais Yoon hapo Jumamosi, wakiita sheria yake ya kijeshi ya muda mfupi kuwa ni tamko la "kinyume cha katiba, uasi haramu au mapinduzi." Lakini  upinzani wenye viti 192 katika Bunge la Kitaifa lenye wabunge 300, wanahitaji kuungwa mkono na wabunge wa chama tawala.

Jaribio la rais Yoon kuanzisha sheria ya kijeshi lilishtua nchi, washirika wa Korea Kusini na masoko ya fedha. Alilitengua muda mfupi baada ya wabunge wa nchi hiyo kupitisha haraka sheria ya kuzuia tangazo hilo.