1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID-19: Karantini yaanza Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
16 Desemba 2020

Ujerumani Jumatano hii imeanza zoezi la kuiweka nchi nzima katika hali ya kufunga shughuli nyingi za kila siku hadi tarehe 10 mwezi ujao kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3mn1m
Deutschland Behandlung eines Patienten auf Intensivstation für Covid-Patienten
Picha: Florian Bachmeier/imageBROKER/picture alliance

Watu wengine 952 wamekufa leo kutokana na maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani. Taarifa hiyo imetolewa na taasisi ya Robert Koch ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza baada ya maambukizi kuongezeka katika muda wa saa 24 zilizopita.

Taasisi hiyo imesema watu 27,728 wameambukizwa na hivyo kufanya idadi ya maambukizi kufikia takriban watu alfu 30 kwa siku tangu Ijumaa iliyopita. Hadi kufikia leo wagonjwa wamelazwa kwa asilimia 83 ya vitanda kwenye wodi za kuwahudumia wagonjwa mahututi.

Soma Zaidi:Utafiti: Idadi kubwa ya watu kutopata chanjo ya COVID-19 hadi 2022 

Taarifa hiyo imetolewa wakati ambapo hatua ya kuiweka nchi yote kwenye karantini imeanza kutekelezwa leo hadi tarahe 10 ya mwezi ujao. Kampuni na waajiri wametakiwa kuwaruhusu wafanyakazi kufanya kazi kutokea majumbani au kuwapa likizo wafanyakazi wao. Hatua hiyo imepitishwa kwa pamoja baina ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mawaziri wakuu wa majimbo yote 16.

Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn
Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens SpahnPicha: Daniel Karmann/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa taasisi ya Robert Koch mpaka sasa watu 23,427 wameshakufa kutokana na maambikizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani. Idadi ya walioambukizwa imefikia watu 1,379,238 na waliopona ni  takriban milioni moja tangu kulipuka kwa maradhi hayo. Idadi ya maambukizi ilikuwa imedhibitika hapo awali na kupungua miongoni mwa vijana lakini iliendelea kuongezeka miongoni mwa wazee ambao wamo hatarini kuathirika zaidi na maambukizi.

Soma Zaidi: Mataifa yapambana kudhibiti COVID 19

Hata hivyo yapo matumaini baada ya mratibu wa chanjo wa Umoja wa Ulaya kutangaza hatua ya kuidhinisha zoezi la kutolewa chanjo mapema kutokana na shinikizo la waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn. Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya Margaritis Schinas amesema katika mahojiano kwamba chanjo dhidi ya Covid-19 itakuwa ni zawadi muhimu ya Krismasi kwa watu wote wa barani Ulaya.

Ujerumani, Italia, Ufaransa, Uhispania, Ubelgiji, Uholanzi, Luxemburg na Uswisi zimethibitisha kwamba zitashirikiana katika mipango ya chanjo hiyo ya Covid -19.

Vyanzo: AFP/DPA/ https://p.dw.com/p/3mmdV