D-Day: Macron, Biden wakutana na Zelensky
7 Juni 2024Biden aliwasilisha ujumbe huo kwa mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika mkutano wao huko mjini Paris. Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema kifurushi hicho kinajumuisha makombora ya Hawk yanayotumiwa katika mifumo ya ulinzi wa anga, risasi, makombora ya masafa marefu aina ya HIMARS na makombora ya kudungua ndege aina ya Stinger. Msaada huo utatumiwa pia kukarabati mifumo ya gridi ya umeme ya taifa ya Ukraine.
Marekani ni mshirika muhimu zaidi wa Kyiv na msambazaji mkubwa zaidi ya silaha katika vita vyake dhidi ya Urusi. Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Washington imetoa au kuahidi msaada wa kijeshi kwa Ukraine wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 51 tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi Februari mwaka 2022.
Soma pia: Maadhimisho miaka 80 ya D-Day yafanyika Normandy
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alimpokea katika ikulu ya Elysée rais Zelensky ambaye baadaye alipata pia fursa ya kulihutubia Bunge la nchi hiyo na kutoa wito kwa washirika wake wa magharibi kuipitia Kyiv msaada zaidi wa kijeshi huku akipongeza hatua ya Ufaransa kuamua kuipatia Ukraine ndege za kivita chapa Mirage-2000.
Kauli za Zelensky
Rais Zelensky amewaambia wabunge wa Ufaransa kuwa iwapo Putin hatozuiwa, hatokomea Ukraine na ataendelea na uvamizi wake hadi kwenye mataifa mengine ya Magharibi. Zelensky ameshukuru kwa misaada na akasema kama ilivyokuwa miaka 80 iliyopita, ukatili wa Putin kamwe hautakiwi kushinda. Aidha Zelensky amewashukuru washirika wake wa Magharibi na kusisitiza kuwa bado safari ni ndefu:
"Ninashukuru kwa yote mnayoyafanya, na kwa hahika ni mengi mno. Lakini ili kufikiwa amani ya haki, kuna mambo zaidi ambayo ni lazima yafanyike. Na hii wala si lawama, ni ukumbusho tu wa jinsi ya kuushinda uovu. Tunahitaji kufanya zaidi leo kuliko tulivyofanya jana, na hivyo huko mbeleni kuliko wakati wowote, tunaweza kukaribia zaidi amani."
Maadhimisho haya ya kumbukumbu ya miaka 80 tangu vikosi washirika vikiongozwa na Marekani na Uingereza vilipotuwa katika fukwe za Normandynchini Ufaransa, ili kuanza operesheni ya kijeshi ya kulikomboa eneo kubwa la kaskazini na Magharibi mwa Ulaya dhidi ya wanazi wa Ujerumani wakati wa vita vya pili vya dunia. Licha ya askari karibu 150,000 kuwasili Normandy Juni 6 mwaka 1944, vita hivyo vya Pili vya dunia viliendelea hadi Mei mwaka 1945.
Soma pia: Viongozi wa Magharibi wakumbuka D-Day chini ya kivuli cha Ukraine
Licha ya kuwa maadhimisho haya yanakumbushia historia mbaya ya Ujerumani, Kansela Olaf Scholz alikumbusha tu kwamba D-Day haikuwa na manufaa kwa Ufaransa na washirika wengine wa Ulaya wakati huo, bali pia ilikuwa siku ya ukombozi kwa Ujerumani kwa kuwa ilijenga msingi wa uhuru na demokrasia.
(Vyanzo: Mashirika)