EU kuanzisha mawasiliano na utawala mpya wa Syria
17 Desemba 2024Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen amesema Jumuiya hiyo itaongeza misaada kwa Syria lakini wakati huio huo ameonya juu ya hatari ya kuibuka tena kwa makundi ya wanamgambo wenye msimamo mkali wa Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS na amesisitiza kuwa hili lazima lisiruhusiwe kutokea.
Naye Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, ameelezea kuwa Jumuiya hiyo imefanya mazungumzo yenye tija na uongozi mpya wa Syria katika hatua ambayo ni muhimu sana.
Soma Pia: Baada ya Syria, je, utawala wa Iran utafuata na kuanguka?
Kallas, amedokeza kwamba Umoja wa Ulaya utatazama upya vikwazo vilivyowekwa kwa Syria ili kuisaidia nchi hiyo katika kipindi cha mpito ikiwa uongozi mpya utachukua hatua kuelekea kuunda serikali jumuishi.
Watawala wapya wa Syria wanaendeleza mashauriano na nchi ambazo zinampinga rais aliyepinduliwa Bashar al-Assad, huku Ufaransa ikipandisha bendera yake kwenye ubalozi wake kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha muongo mmoja.
Uturuki na Qatar, ambazo ziliunga mkono upinzani dhidi ya Assad, pia zimefungua tena balozi zao mjini Damascus, wakati huo huo maafisa wa Marekani na Uingereza wameanzisha mawasiliano na viongozi wapya wa Syria.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema Umoja wa Falme za Kiarabu unawashuku viongozi wapya wa Syria, na kuonyesha kutokuwa na imani na siasa zinazochanganya dini na pia una hofu ya ushawishi mkubwa wa Uturuki katika nchi hiyo ya Syria iliyokumbwa na vita.
Soma Pia: Kiongozi wa Syria asema makundi ya waasi "yatavunjwa"
Baada ya kuwa na uhusiano mkubwa na Bashar al-Assad, Umoja wa Falme za Kiarabu umepata pigo kubwa kwa kuondolewa kwa mtawala huyo wa muda mrefu katika mashambulizi yaliyoongozwa na kundi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS).
Wakati hayo yakiendelea Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi limesema linatarajia Wasyria milioni 1 kurejea nchini Syria katika miezi sita ya kwanza ya mwaka ujao wa 2025.
Rema Jamous Imseis, Mkurugenzi wa UNHCR wa Maeneo ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini amesema kutokana na utabiri huo wameuhusisha mpango huu wa wasirya kurejea nyumbani na wafadhili, na kuwaomba msaada wao.
Amesema maelfu ya watu wanaorejea nchini Syria baada ya waasi kuchukua mamlaka kutoka kwa Rais Bashar al-Assad, wanatokea katika nchi za Uturuki, Lebanon na Jordan.
Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, ametangaza kwamba Uturuki itapokea nyongeza ya dola bilioni 1.05 kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Syria katika nchi hiyo.
Vyanzo: RTRE/AFP/DPA